Rais Dkt.Mwinyi amshirikisha jambo Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za Kitaifa ya Oman

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameiomba Serikali ya Oman kusaidia upatikanaji wa mafunzo kwa watendaji wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akipata maelezo ya moja ya kitabu kinachoelezea historia na kumbukumbu ya Oman na Zanzibar kutoka kwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za Kitaifa ya Oman, Dkt. Hamed Mohd Al Dhawiani, wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo. (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Dkt.Mwinyi ametoa ombi hilo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za Kitaifa ya Oman, Dkt. Hamed Mohd Al-Dhawiani aliyefika nchini kwa lengo la kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, hususani katika suala la uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu za Taifa.

Amesema, kuna umuhimu kwa Taifa la Oman kusaidia upatikanaji wa mafunzo kwa watendaji wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar ili kuwajengea uwezo.

Amesema, hatua hiyo itawawezesha watendaji hao kufanya kazi kwa weledi na ufanisi, hususan pale Zanzibar itakapofanikiwa kuwa na Kituo cha Maonyesho (exhibition centre).

Aidha, alisema Zanzibar iko tayari kuendeleza uhusiano na ushirikiano na Oman katika uimarishaji wa hifadhi za nyaraka na kumbukumbu ziliopo ili iweze kufikia kiwango cha kuwa na ‘Exhibition centre’ kama ilivyo kwa miji ya Lamu na Mombasa, nchini Kenya.

Amesema mafanikio hayo yatasaidia uhifadhi bora wa historia ya Zanzibar, hususani kwa watu wanaokuja kujifunza au kufanya tafiti mbalimbali.

Naye Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za Kitaifa ya Oman, Dkt. Al- Dhawiani amesema katika kuendeleza ushirikiano na Zanzibar, Oman imetenga bajeti maalumu kwa ajili ya kusadia uwekaji wa mazingira bora katika maeneo ya uhifadhi wa Nyaraka na Kumbukumbu ziliopo, huku akibainisha umuhimu wake katika kusaidia watu wenye mahitaji ya kufanya tafiti.

Amesema, pia Oman inalenga kuendeleza programu ya kuwapatia mafunzo watendaji wa taasisi hiyo ili kuwa katika nafasi nzuri ya kiutendaji.

Alieleza kuwa, Oman ina uzoefu mkubwa katika suala la uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu, ambapo watendaji kutoka mataifa mbalimbali duniani yakiwemo ya Bara la Afrika wamekuwa wakifika nchini humo kwa ajili ya kujifunza.

Amesema, Oman haina dhamira ya kuhodhi nyaraka ama kumbukumbu zilizopo hapa nchini na kusema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia nyaraka zake.

Dkt.Al-Dhawiani amesema, Oman na Zanzibar zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao kamwe hauwezi kuvunjika kwa vile unatokana na misingi ya dini, mila, lugha pamoja na watu wa pande mbili hizo kuchangiana damu pamoja na kutembeleana.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Jamal Kassim Ali alizungumza na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za kitaifa ya Oman, Dkt. Al-Dhawiani na kusema kumbukumbu za Zanzibar ni sehemu muhimu ya urithi wa Dunia, zikiwa na umuhimu mkubwa kwa vizazi vijavyo.

Alieleza kuwa, ushirikiano unaoendelea kati ya Oman na Zanzibar utatoa fursa ya kuimarisha uhifadhi bora wa nyaraka na kumbukumbu za Taifa.

Aidha, amesema ujio wa ujumbe huo kutoka Oman utakuwa wa manufaa makubwa katika majadiliano yatakayofanyika na Uongozi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar na hatimaye kuleta mustakabali mwema kwa mataifa hayo mawili.

Naye Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za Kitaifa ya Oman, Dkt. Al-Dhawiani amesema, nchi hiyo ina matarajio ya kufanya mambo mbalimbali ili kuimarisha uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu za Taifa kama ilivyofanyika nchini Kenya katika Miji ya Mombasa na Lamu.

Aliishauri Serikali kuhifadhi vyema nyaraka zote zilizopo hapa nchini kupitia mfumo wa teknolojia ya kisasa ili ziweze kutumika bila kuwepo changamoto za aina yoyote na kusisitiza umuhimu wa historia kubaki kama ilivyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news