Rais Dkt.Mwinyi:Hongereni JWTZ kwa kusimamia vema ulinzi, usalama nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa kuendelea kusimamia ulinzi na usalama hapa nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 1, 2022 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Haji Othman, aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alimueleza Mnadhimu Mkuu huyo wa JWTZ kwamba, hali ya amani, ulinzi na usalama hapa Zanzibar imezidi kuimarika kutokana na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, hatua za JWTZ ya kuendelea kusimamia ulinzi na usalama wa nchi imepelekea kupatikana kwa mafanikio makubwa.

Hivyo, Rais Dkt.Mwinyi amemuhakikishia Mnadhimu Mkuu huyo wa JWTZ kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na jeshi hilo ili mafanikio zaidi yaendelee kupatikana.

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Mwinyi amempongeza Luteni Jenerali Othman kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kumuahidi kwamba ataendelea kushirikiana nae ili aendelee kufanya kazi zake katika kulitumikia jeshi hilo kwa ufanisi zaidi.

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alieleza haja ya kuendeleza ushirikiano na Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) na kusema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano na chuo hicho ambacho kila mwaka wahitimu wake wamekuwa wakifika Zanzibar ikiwa ni sehemu yao ya masomo.

Mapema Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Haji Othman alimueleza Rais Dkt.Mwinyi kwamba uteuzi wake katika nafasi hiyo ulifanyika tarehe 30 Juni 2022 baada ya aliyekuwa Mnadhimu Mkuu Luteni Jenerali Mathew Mkingule kupangiwa majukumu ya Ubalozi nchini Zambia.

Hivyo, alimueleza Rais Dkt.Mwinyi kwamba kufuatia kuteuliwa kwake ameona ni vyema aje kumsalimia pamoja na kujitambulisha kwake na kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mnadhimu Mkuu huyo alieleza jinsi anavyotambua mchango mkubwa wa Rais Dkt.Mwinyi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa JWTZ.

“Mheshimiwa Rais umekuwa karibu sana na jeshi letu, kwa ushauri na kwa nasaha zako zilizojaa hekima na busara nyingi ulizojaaliwa na Mwenyezi Mungu, JWTZ siyo taasisi ngeni kwani kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa umeliongoza jeshi hili kwa miaka kumi katika mazingira haya sidhani kama kuna jambo jipya nitakaloweza kukueleza ukawa hulifahamu kuhusu JWTZ na sekta nzima ya ulinzi kwa ujumla wake,”alisema Mnadhimu Mkuu huyo wa JWTZ.

Aidha, Luteni Jenerali Othman alieleza jinsi, Rais Dkt.Mwinyi kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anavyosaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta utangamano kati ya wananchi na jeshi lao kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi na kusaidia kupata ufumbuzi wa kudumu.

Luteni Jenerali Othman alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kuendeleza ukaribu wake na Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) ikiwa ni pamoja na kuwakaribisha washiriki wa kozi hiyo kuja Zanzibar pamoja na kuwafanyia mhadhara hapo Ikulu.

Katika maelezo yake Mnadhimu Mkuu huyo alieleza kwamba tayari ameshanza shughuli zake za kazi na kwa mara ya kwanza ameanza kisiwani Pemba kwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi pamoja na maafisa wa jeshi hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news