Rais Dkt.Mwinyi:Vijana tumieni mabaraza yenu kama chemchem ya fikra, kupaza sauti

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka vijana kuendelea kuyatumia mabaraza yao kama chemchem ya fikra mpya na jukwaa la kupaza sauti zao katika masuala muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Vijana Kimataifa, maadhimisho hayo yamefanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Unguja jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Dkt.Mwinyi ametoa wito huo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Kikwajuni jijini Zanzibar.

Amesema, Serikali imeelekeza juhudi kubwa katika kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za ujenzi wa Taifa kupitia Baraza la Vijana Zanzibar, kwa kigezo kuwa ndio sehemu maalum itakayowawezesha kukutana na kujadili masuala mbalimbali yatakayosaidia nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Akinukuu hotuba za Rais wa Kwanza wa Zanzibar na mwasisi wa Mapinduzi, Hayati mzee Abeid Amani Karume, Dkt. Mwinyi amehimiza umuhimu wa vijana kujiamini, kuacha ubinafsi, kuwa wabunifu na kuwa wazalendo ili kutimiza malengo ya Mapinduzi ya 1964.

Amesema, ni muhimu kuweka mazingatio ya mambo hayo kwa kuzingatia umuhimu wake katika kujenga mshikamano wa kweli kati yao na wananchi wote wa Zanzibar.

“Tuhakikishe mipango na matendo yetu yanazingatia maslahi mapana ya Taifa letu,"amesisitiza Rais Dkt.Mwinyi.

Akigusia ujumbe wa maadhimisho hayo usemao, ‘Mshikamano baina ya Vizazi ili kujenga Dunia ya rika zote’, Rais Dkt.Mwinyi amesema, ujumbe huo ni muhimu kwani unahimiza umoja na mshikamano baina ya watu wa rika zote kwa misingi ile ile iliyohimizwa na waasisi wa Taifa pamoja na miongozo ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Dkt.Mwinyi amesema, Serikali imeongeza juhudi katika kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia mitaji, elimu ya ujasiriamali pamoja na kuongeza fursa za masoko na kuhimiza dhana ya kuwaelimisha wajasiriamali umuhimu wa kuelekeza nguvu katika kutafuta masoko na kuzalisha bidhaa bora zinazohitajika katika Sekta ya Utalii.

Amesema, Serikali imetenga kiwango kikubwa cha fedha kupitia Mkopo wa Ahueni ya Uviko -19 kwa ajili ya kuwaendeleza wajasiriamali wanaojishughulisha na sekta za kilimo cha mwani, uvuvi, utalii, utengenezaji wa bidhaa mbalimbali pamoja na wasanii wa kazi za mikono.

Amesema, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inatengeneza mazingira yatakayovutia zaidi vijana kupenda kujiajiri kwa kutambua maendeleo ya sekta binafsi ndio msingi mkuu wa ajira katika Taifa lolote lile.

Amesema, Serikali inaendelea kupanga na kutekeleza miradi mikubwa katika ujenzi wa miundombinu, kuendeleza uchumi wa Buluu, kuimarisha utalii, uwekezaji na biashara ili kutanua wigo wa upatikanaji wa fursa kwa vijana na kukuza uchumi wa Taifa.

Amewataka vijana hao kuendeleza mafanikio makubwa yaliofikiwa na kusema Serikali inathamini sana juhudi hizo, hususan katika kuendeleza na kukuza sanaa, utamaduni na michezo.

Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Timu ya Riverside ya Jang’ombe kwa kutwaa Ubingwa wa Ligi ya Vijana pamoja na kuzipongeza Timu za KMKM kwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar pamoja na Timu ya Jeshi ya Kipanga kwa kubeba Taji la FA Cup.

Aidha, alizipongeza na kuzitakia mafanikio mema timu za Jamhuri na Chipukizi kutoka Pemba kwa kupanda Daraja na kuingia Ligi Kuu ya Zanzibar pamoja na Timu za Kundemba ya Mjini Unguja na Dulla Boys ya Jambiani kwa upande wa Zanzibar.

Katika hatua nyingine, aliwataka vijana kuwa wabunifu, wajasiri na walio na utayari katika kufanya mambo mapya.

Aliwataka kuhakikisha wanatekeleza vyema jukumu la kulinda na kuendeleza amani pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa makundi yote ndani ya jamii.

Katika hafla hiyo Dkt.Mwinyi alipata fursa ya kukabidhi Mfano wa Hundi ya Shilingi Milioni 15 kutoka Shirika linaloshughulikia changamoto za Vijana (IRI) kwa ajili ya vijana tisa pamoja na mfano wa hundi ya shilingi Milioni 50 kutoka Youth Challenge International Tanzania kwa ajili ya vijana 18 baada ya kupata mafunzo.

Mapema, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita alisema wizara hiyo inaendelea kuwajengea mazingira bora vijana kisera na miundombinu wezeshi pamoja na mambo mbalimbali ili kukuza ushiriki na ushirikishwaji.

Alisema, wizara hiyo ina mipango ya kujenga vituo vya mafunzo kwa vijana katika maeneo ya Bweleo Mkoa Mjini Magharibi na Weni Kisiwani Pemba katika nyanja za ushoni, ujasiriamali, stadi za maisha ikiwa ni hatua ya kusaidia utoaji nasaha na kuwawezesha kumudu maisha.

Aidha, alisema wizara ina azma ya kujenga vituo vya ufugaji kupitia fedha za ahueni ya mfuko wa Uviko-19 katika maeneo ya Pangeni Unguja pamoja na Ole kisiiwani Pemba.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar, Yunus Juma Ali alimhakikishia Rais Dkt.Mwinyi kuwa Baraza hilo litaendelea na kazi za kuwahamasisha wananchi katika mikoa yote ya Unguja kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Dkt.Mwinyi kwa kuimarisha uchumi wa Zanzibar pamoja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suliuhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuiongoza Tanzania.

Aidha, aliwasilisha ombi la baraza hilo kwa Rais Dkt.Mwinyi la kumuomba kushirki katika maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani, kila mwaka katika kipindi chote cha uongozi wake.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani hufanyika kila ifikapo Agosti 12 ya kila mwaka, ikiwa ni hatua ya kufanya tathmini ya mafanikio ya vijana katika juhudi zao za ujenzi wa Taifa pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news