Rais Samia alitaka Jeshi la Magereza kurekebisha tabia za wafungwa

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Magereza kuhakikisha linafanya kazi ya msingi ya kurekebisha tabia za wafungwa.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo Ikulu Chamwino katika hafla ya kumuapisha Kamishna Jenerali wa Magereza CGP Mzee Ramadhani Nyamka pamoja na Majaji 21 wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Aidha, Rais Samia amesema wafungwa wakipata marekebisho ya tabia yatawasaidia kuwa waadilifu na kulitumikia taifa pindi wanapomaliza vifungo vyao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Mzee Ramadhani Nyamka kuwa Mkuu wa Jeshi hilo katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 29 Agosti, 2022.

Rais Samia ametoa wito kwa Magereza kuwatendea haki wafungwa kwa kulinda maisha na haki zao pamoja na kuzingatia mahitaji yao.

Vile vile, Rais Samia amemtaka Kamishna Jenerali wa Magereza kurekebisha changamoto za kiutawala katika Jeshi la Magereza pamoja na kusimamia haki za watumishi katika Jeshi hilo.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Majaji aliowaapisha kufanya kazi kwa uadilifu pamoja na kufuata mila na desturi za Kitanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Mzee Ramadhani Nyamka mara baada ya hafla ya Uapisho iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 29 Agosti, 2022.

Halikadhalika, Rais Samia amewataka Majaji hao kutenda haki kwa wananchi wakati wa kutoa hukumu.

Post a Comment

0 Comments