Rais Samia aomboleza kifo cha Dkt.Mrema

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameelezea kupokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwenyekiri wa Chama cha TLP, Dkt.Agustino Lyatonga Mrema.

Dkt.Mrema ambaye alizaliwa Desemba 31, 1944, Vunjo mkoani Kilimanjaro kwa mujibu wa taarifa ya     Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Buberwa Aligaesha alilazwa hospitalini hapo kuanzia Agosti 16,2022 na kufikwa na mauti asubuhi ya leo Jumapili Agosti 21,2022 saa 12:15.

Mheshimiwa Rais Samia kupitia taarifa aliyoitoa leo Agosti 21, 2022 ameeleza kuwa, ataendelea kumbukumbuka Dkt. Mrema kwa mambo mengi.

"Nimesikitishwa na kifo cha Mwenyekiti wa chama cha TLP Bw. Agustino Lyatonga Mrema kilichotokea leo asubuhi Jijini Dar es Salaam. Nitamkumbuka kwa mchango wake katika mageuzi ya siasa, uzalendo na upendo kwa Watanzania. Pole kwa familia na wana TLP. Mungu amweke mahali pema.Amina,"ameeleza Mheshimiwa Rais Samia.

Dkt.Mrema wakati wa uhai wake amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, mgombea urais kupitia NCCR-Mageuzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 baada ya kujiunga na chama hicho akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pia amewahi kuwa Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Temeke (NCCR Mageuzi) na Vunjo kupitia TLP na hadi amefikwa na mauti alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.

Parole ni nini?

Bodi ya Taifa Parole ni tasnia muhimu sana katika urekebishaji wa wahalifu kwa kuishirikisha jamii. Tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo mwaka 1994, mafanikio makubwa yameonekana kutokana na baadhi ya wafungwa kuachiliwa kupitia utaratibu huo, hivyo kupunguza sehemu ya changamoto ya msongamano magerezani.

Post a Comment

0 Comments