Rais wa Yanga SC Mhandisi Hersi Said, Haji Manara wafunguliwa mashtaka

NA GODFREY NNKO

SEKRETARIETI ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafunguliwa mashtaka ya kimaadili Rais wa Klabu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said na aliyekuwa afisa wa klabu hiyo, Bw.Haji Manara.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 7, 2022 kwa umma na Afisa Habari na Mawasiliano wa shirikisho hilo, Bw.Cliford Mario Ndimbo.

"Kamati ya Maaadili ya TFF hivi karibuni ilimfungia miaka miwili, Bw.Haji Manara kutojihusisha na shughuli yoyote ya mpira wa miguu (any football-related activity), lakini ameshindwa kutekeleza adhabu hiyo,"ameeleza Bw.Ndimbo.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mhandisi Said naye amefunguliwa mashtaka ya kwenda kinyume na Ibara ya 16 (1) (a) ya Katiba ya TFF, pamoja na Ibara ya 1 (6) ya Katiba ya Yanga.

"Baada ya Manara kuadhibiwa na Kamati ya Maadili ya TFF, Sekretarieti ilimwandikia barua Mhandisi Said kuhakikisha klabu yake inaheshimu uamuzi.

"Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF tayari amepelekewa mashtaka hayo, walalamikiwa watapewa mashtaka na wito baada ya kamati hiyo kupanga tarehe ya kusikiliza mashtaka hayo,"amefafanua Bw.Ndimbo kupitia taarifa hiyo.

Post a Comment

0 Comments