Riadha ni miongoni mwa michezo ya kipaumbele-Mheshimiwa Gekul

NA ELEUTERI MANGI

NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amesema Serikali imejipanga kuendeleza mchezo wa riadha ambao ni miongoni mwa michezo ya kipaumbele hatua itakayosaidia kupata wanariadha watakaowakilisha nchi Kimataifa.
Naibu Waziri Gekul amesema hayo wakati akizindua Mbio za Kimataifa za Tanzanite Manyara (Manyara Tanzanite International Marathon) katika Uwanja wa Kwaraa Agosti 13, 2022 mjini Babati.

“Tumeanza safari ya kuibua vipaji vya wanariadha kwa Halmashauri ya mji wa Babati, wilaya zote za mkoa wa Manyara, hatimaye safari hii inalenga kufikia mikoa mitano ya kimkakati katika mchezo wa riadha ambayo ni Arusha, Singida, Manyara, Mara na Mbeya,”amesema Naibu Waziri Gekul.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Lazaro Twange amewahimiza wananchi kushiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ambayo itafanyika Agosti 23, 2022 ili nchi iweze kuweka mipango ya kuwapatia huduma watu wake kwa maendeleo endelevu.

Mbio za Manyara Tanzanite Internatinal Marathon za mwaka huu wa 2022 zimeshirikisha wanariadha katika mbio za uwanjani Mita 100, 400, 800 na 1500 pamoja na mbio ndefu za kilometa 5, 10 na 21 huku mshindi wa KM 21 wanaume Elisha Wema ambaye alikimbia kwa saa 1:05:37 akisema mashindano hayo yanatoa nafasi kwa vijana wengi kuonesha vipaji vyao.

Post a Comment

0 Comments