Waziri Bashungwa atoa maagizo nane kwa wakuu wote wa mikoa nchini

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imetoa maagizo nane kwa wakuu wa mikoa yote nchini ambayo yanapaswa kutekelezwa kikamilifu ili kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.
Maagizo hayo yametolewa na Waziri Innocent Bashungwa leo Agosti 2, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu mapato na matumizi ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

"Hakikisheni wakurugenzi wa halmashauri wanawalipa wakusanya mapato posho zao kwa wakati na kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinakwenda benki kwa wakati na kuondoa mianya yote ya upotevu wa mapato ikiwemo watumishi kushirikiana na wakusanya mapato kufanya udanganyifu.

"Aidha, yeyote anayecheza na mifumo ya ukusanyaji mapato achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo,"amesema Waziri Bashungwa.

Jambo la pili ni pamoja na wakuu wa mikoa kuhakikisha halmashauri zilizopo zote zinahuisha Leseni za Biashara ili kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani.

Aidha, amesema zipo baadhi halmashauri huku akitolea mfano halmashauri za wilaya za Kilosa na Kiteto ambazo kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya mwaka 2020/21 hazikuhuisha Leseni za Biashara hali iliyosababisha zikakosa mapato.

"Jambo la nne wakuu wa mikoa wanapaswa kuhakikisha makisio ya bajeti za mapato ya ndani ya halmashauri zinazingatia uhalisia wa vyanzo vya mapato ili kuwa na maoteo halisi.

"Mfano, katika taarifa (aliyoiwasilisha) hii zipo halmashauri ambazo zimekusanya zaidi ya asilimia 100, lakini hazikuwahi kuomba kuhuisha bajeti zao ili ziendane na uhalisia kama vile halmashauri za Wilaya za Kibaha, Mlele na Halmashauri ya Mji wa Mbulu.

"Pia zipo halmashauri ambazo ziliomba kupunguza bajeti zao hata hivyo, mwisho wa mwaka zimekusanya zaidi ya asilimia 100 kama vile Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

"Na zipo halmashauri ambazo zimeomba kuongeza bajeti zaidi ya mara moja katika mwaka kama vile halmashauri za Wilaya za Morogoro, Rufiji, Kaliua na Nyang’hwale hata hivyo bado zimekusanya zaidi ya asilimia 100.

"Hali hili inaashiria kwamba halmashauri bado zina fursa ya kukusanya mapato isipokuwa haziko makini katika kuchambua uhalisia wa kila chanzo ili kupata makisio halisi na hivyo kuamua kuweka kiasi chochote wanachofikiria,"ameelekeza Waziri Bashungwa.

Agizo la nne, Waziri Bashungwa amesema halmashauri zihakikishe fedha zilizovuka mwaka wa fedha 2021/22 (Bakaa) zinatumika kabla au ifikapo tarehe 30 Septemba, 2022 kwa kufuata Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo.
"Katika eneo hili naelekeza halmashauri zote zenye Bakaa ziwasilishe orodha ya miradi itakayotekelezwa kwa fedha hizo kupitia mikoa na ufanyike ufuatiliaji wa fedha hizo na kunipa taarifa ambayo nitaitoa kwa wananchi wakati nitakaposoma taarifa ya robo ya kwanza mwaka 2022/23,"ameeleza Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Katika agizo la tano, Waziri Bashungwa amewataka wakuu wa mikoa kuhakikisha halmashauri zote zinatekeza mapendekezo na kufunga hoja zote za ukaguzi zilizotolewa na CAG.

"Aidha, nasisitiza hili lifanyike pia kwa hoja za Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ambapo kule kumekuwepo na hoja nyingi ambazo hazijafungwa na hoja hizo zimekuwa zikijirudia pia kwenye hoja za CAG,"amesema Mheshimiwa Waziri.

Agizo la sita, Mheshimiwa Waziri amewataka wakuu wa mikoa kuhakikisha halmashauri ambazo hazikufanikiwa kukamilisha utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi yaliyotolewa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 zinakamilisha maagizo hayo kabla au ifikapo tarehe 30 Septemba,2022 na kutoa taarifa Ofisi ya Rais- TAMISEMI.

Mheshimiwa Waziri Bashungwa katika agizo la saba amesema, wakuu wa mikoa wanapaswa kusimamia ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye ngazi za kata na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha zinazotoka Serikali Kuu na fedha za mapato ya ndani zinazoelekezwa kwenye ngazi ya kata ili kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa kwenye miradi yenye tija kwa wananchi.

"Agizo la nane ni kuhakikisha ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri unajumuisha ukaguzi wa Miradi inayotokana na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

"Aidha, mikoa ibainishe kiasi chote cha fedha za mikopo ya asilimia 10 ambacho hakijarejeshwa na kusimamia urejeshaji na kuwasilisha taarifa Ofisi ya Rais-TAMISEMI,"amefafanua Mheshimiwa Waziri.

Kuhusu agizo hilo, Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema Mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi wa mikopo hiyo upo tayari na umeanza kutumika katika halmashauri zote.

"Ninaelekeza mkazisimamie halmashauri zote na kuhakikisha vikundi vyote vilivyowahi kupata mikopo na havijamaliza marejesho vinaingizwa kwenye mfumo na kazi ya kuingiza taarifa za vikundi hivyo iwe imekamilika ifikapo tarehe 30 Agosti, 2022.

"Na Katibu Mkuu atasimamia hili kuanzia Agosti Mosi, mwaka huu kuona ni halmashauri zipi zinatekeleza na ambazo hazifanyi chochote tutachukua hatua kwa kuwa tutakuwa na uwezo wa kuona kupitia kwenye mfumo.

"Watakwimu katika halmashauri na mikoa watumike ipasavyo. Serikali haitavumilia kuona bado kuna fedha zisizorejeshwa au mikopo kutolewa kwa vikundi hewa au wanufaika wasiostahili. Ninapenda kusisitiza tena, wakuu wa mikoa hakikisheni mikopo yote inarejeshwa. Tufuate mfano wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza katika kusimamia fedha za mikopo,"amesema Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news