Waziri Mkuu akagua ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida

NA DIRAMAKINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na kusema kwamba mradi huo ni ukombozi kwa wakazi wa mkoa huo na jirani.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Dkt. Deogratias Banuba (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa hospitali hiyo ya Rufaa, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Singida. Agosti 6, 2022.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anaridhia ujenzi wa miradi hii ili kuhakikisha Watanzania hawatumii gharama kubwa kwenda mbali kufuata huduma mbalimbali.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Agosti 6, 2022 baada ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo ambao unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 19.

Amesema hospitali hiyo itakapokamilika mbali na kuhudumia wananchi wa mkoa wa Singida, pia wakazi wengine wa mikoa ya jirani ya Manyara, Simiyu na Tabora nao watanufaika.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Dkt. Deogratias Banuba amesema kukamilika kwa hospitali hiyo kutaimarisha utoaji wa huduma za afya.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Singida, ambalo ujenzi wake unategemea kukamilika ifikapo Novemba, 2022, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Singida.

Mapema, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Ester Chaula ahakikishe ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo linalojengwa katika kata ya Ilongero unakamilika ili wananchi wapate huduma.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo, ambapo amesema ameridhishwa na hatua ya ujenzi wa jengo hilo ambalo linatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi huyo asimamie vizuri idara ya manunuzi ili inunue vitu kwa bei halisi na mjenzi aweze kukamilisha ujenzi kwa wakati.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Singida, ambalo ujenzi wake unategemea kukamilika ifikapo Novemba, 2022, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Singida.

Kwa upande wake, Mkurugebzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Ester amesema ujenzi wa jengo unajengwa kwa awamu mbili kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.7.

Amesema awamu ya kwanza umefikia hatua ya umaliziaji sawa na asilimia 92 na awamu ya pili umefikia hatua ya ujenzi wa ghorofa ya kwanza sawa na asilimia 45.

Naye, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI, David Silinde amesema ujenzi wa jengo hilo ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Singida, ambalo ujenzi wake unategemea kukamilika ifikapo Novemba, 2022, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Singida.

Naibu Waziri huyo amesema Mheshimiwa Rais Samia aliagiza ujenzi wa majengo ya utawala katika halmashauri zote zisizo na majengo ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Naye, Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Singida, Nusrat Hanje amewataka wakazi wa mkoa huo waendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia katika kuliletea Taifa maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news