eGA yawapatia mafunzo ya TEHAMA vijana wa vyuo vikuu


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imewapatia mafunzo ya TEHAMA vijana wa vyuo vikuu ili kuwajengea uwezo utakaosaidia kuleta maendeleo ya TEHAMA nchini ikiwa ni pamoja na kuwaandaa vijana hao kutoa mchango katika utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.

Mhe. Ndejembi amesema hayo jijini Dodoma, wakati akifunga mafunzo ya TEHAMA kwa vijana hao wa vyuo vikuu yanayotolewa kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Naibu Waziri Ndejembi amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeelekeza nguvu nyingi katika utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambao unahitaji wataalam na ndio sababu ya serikali kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa vijana ya vyuo vikuu.

“Ninyi vijana mliopatiwa mafunzo kupitia kituo hiki cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha eGA ndio wataalam mnaotegemewa kutoa mchango ili kufikia lengo la Mhe. Rais la kuwa na Tanzania ya Kidijitali,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Post a Comment

0 Comments