Makamu wa Rais Dkt.Mpango ahutubia Mkutano wa Elimu wa Umoja wa Mataifa

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amehutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mageuzi katika sekta ya elimu wa Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, Wakuu wa Taasisi na Mashirika na wadau wa elimu.
Akizungumza katika Mkutano huo Mhe. Dkt. Mpango amesema Mataifa yanapaswa kujitoa upya na kuongeza uwekezaji zaidi katika sekta ya elimu ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na ya uhakika katika kuelekea mwaka 2030.

Amesema elimu ni sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo 2030 hivyo ni lazima kuchukua hatua kuleta mabadiliko kwenye sekta hiyo na kuongeza kuwa kupatikana kwa elimu bora kutapunguza matabaka katika ajira pamoja na kipato baina ya wananchi.

Amesema Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha sekta ya elimu ikiwemo kuanza mchakato wa kuboresha mitaala kwa kuwashirikisha wadau wa elimu, kuwekeza katika vyuo vya ufundi stadi na mafunzo , kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuongeza bajeti ya wizara husika kufikia asilimia 18 ya bajeti yote ya serikali.

Amesema Serikali ya Tanzania inahakikisha upatikanaji wa elimu jumuishi kwa wote bila kujali jinsia , ulemavu na hali ya uchumi na kwa kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia Serikali pia imedhamiria kuboresha usimamizi wa nguvu kazi ya walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji bora kwa kuwajengea uwezo walimu na maofisa elimu kuhusu uunganishaji wa teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji na uandaaji wa masomo ya kidijitali.
Makamu wa Rais Dkt. Mpango, yupo nchini Marekani kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news