NCHI ZETU ZIMESEMA: LINAJENGWA BOMBA LETU

NA LWAGA MWAMBANDE

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema inasimamia kikamilifu sekta ya nishati, ikiwemo kuendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani jijini Tanga ili kukuza uchumi.

Aidha, kutokana na hali hiyo, Serikali imewahakikishia wadau mbalimbali kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia sheria zote za Tanzania na za kimataifa, uwazi na tahadhari za kimazingira.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo Septemba 23,2022, wakati akiahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma.

Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema baadhi ya wadau wa maendeleo wamekuwa na mashaka katika utekelezaji wa mradi huo, wakihofia kuwa unaweza kutekelezwa pasipo kuzingatia athari za kimazingira na haki za binadamu.

Amesema, mradi huo umefanyiwa tathmini ya kina ya kimazingira na kuhakikisha kuwa utekelezaji wake hauna athari za kimazingira na kwa jamii. Ili uweze kufahamu zaidi, ungana na mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande kupitia shairi hapa chini;

1:Nchi zetu zimesema, linajengwa Bomba letu,
Toka Uganda Hoima, hadi Tanga hapa kwetu,
Kidete zimesimama, huo msimamo wetu,
Wengine wenye mashaka, hebu tuache kidogo.

2:Bomba la Mafuta Ghafi, yaliyoko kanda yetu,
Yatasafirishwa safi, hadi bandarini kwetu,
Asitokee mlafi, kukatiza mambo yetu,
Wengine wenye mashaka, hebu tuache kidogo.

3:Hao na maneno yao, kwao wala siyo kwetu,
Wanayo mabomba yao, sisi hatusemi kitu,
Hili letu siyo lao, kelele ni nyingi kwetu,
Wengine wenye mashaka, hebu tuache kidogo.

4:Kulijenga Bomba hili, tunayo malengo yetu,
Mafuta haya ni mali, kwa huu uchumi wetu,
Hata na ujenzi mali, waleta ajira kwetu,
Wengine wenye mashaka, hebu tuache kidogo.

5:Maswala ya kimazingira, kati yenu na ya kwetu,
Nani aleta hasara, kubwa duniani kwetu?
Mbona makubwa madhara kwenu kunazidi kwetu?
Wengine wenye mashaka, hebu tuache kidogo.

6:Tulikwishajiandaa, tukijua hali yetu,
Maeneo yanafaa, ya kupita bomba letu,
Yale watu wanakaa, ni maandalizi yetu,
Wengine wenye mashaka, hebu tuache kidogo.

7:Hii sasa zamu yetu, ushirikiano wetu,
Tunafanya jambo letu, kwa maendeleo yetu,
Umoja ni nguvu zetu, na mafanikio yetu,
Wengine wenye mashaka, hebu tuache kidogo.

8:Nyie Bunge la Ulaya, fanya yenu haya yetu,
Na tena muone haya, kutufwatafwata kwetu,
Mambo ya huko Ulaya, mbona hatusemi kwetu?
Wengine wenye mashaka, hebu tuache kidogo.

9:Uganda na Tanzania, tuzidi fanya ya kwetu,
Ile tumeweka nia, iwe akilini mwetu,
Wale wanaingilia, washindwe umoja wetu,
Wengine wenye mashaka, hebu tuache kidogo.

10:Wenye wana boriti, wadai kibanzi kwetu,
Watoe zao boriti, ndiyo wasogee kwetu,
Hii yetu mikakati, tafika malengo yetu,
Wengine wenye mashaka, hebu tuache kidogo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments