TUUCHAGUE MFUMO-1:Tuzijenge timu zetu, kwa maendeleo yetu

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, mpira wa miguu ndiyo mchezo unaoongoza duniani. Lakini siku zote unahitaji msaada wa kila mmoja kuufanya uendelee kuwa mchezo wenye kupendwa zaidi.
Kwanza, soka inachezwa kwa urahisi kwenye mazingira yoyote. Tofauti na hata mchezo wa Baseball,soka huwa inavutia wengi hata uwekezaji katika upande huo ni mkubwa kwa kuwa ni sehemu unayoweza kuwekeza na ukapata faida au kurejesha gharama zako mapema.

Pili, utangazaji na ufadhili ni mkubwa sana katika nchi nyingi duniani. Tatu, nchi chache zina mchezo mwingine wa kitaifa unaofaa huku soka ikiwa namba moja.

Kwa Tanzania, soka ni miongoni mwa michezo pendwa ambayo imekuwa ikiwavutia maelfu ya mashabiki, ndiyo maana kwa kutambua umuhimu wake, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,yafaa sasa hapa kwetu tuchague mfumo ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa soka la Tanzania, kwani uchaguzi ni wa kwetu, jifunze kitu kupitia shairi hapa chini;

1.Uchaguzi ni wa kwetu, Marekani kuwe kwetu,
Uingereza si kwetu, au huko kuwe kwetu,
Tuzijenge timu zetu, kwa maendeleo yetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

2.Marekani timu zao, wala si kama za kwetu,
Na hata mabingwa wao, siyo kama timu zetu,
Wameendelea wao, si London sio kwetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

3.Soka lipo hapa kwetu, lina sifa sana kwetu,
Marekani siyo kwetu, michezo yao si yetu,
Kwao kuna kitu chetu, kwa maendeleo yetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

4.NBA ni kwatu, Marekani kuna watu,
NFL watu, tunawasikia watu,
Baseball nao kitu, jinsi wachezwa na watu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

5.Uingereza na kwetu, kwa sasa kama ni kwatu,
Timu zao timu zetu, wanajipigania tu,
Maarufu ni nyingi tu, zenye mavitu na vitu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

6.Uingereza na kwetu, tajiri ni timu zetu,
Masikini pia zetu, zinazoungaunga tu,
Tunaona roho kwatu, kwamba zitambe chache tu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

7.Uingereza si kwetu, timu kubwa ni chache tu,
Hesabu ziko chache tu, nyingi ni washiriki tu,
Mabingwa kwao na kwetu, kama ni walewale tu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

8.Hapa Simba na Yanga tu, hasa ni mabingwa kwetu,
Zingine mara moja tu, kama kuonjaonja tu,
Sababu ziko wazi tu, peza zao kiduchu tu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

9.Faida ni chache kwetu, hasara ni nyingi kwetu,
Uingereza kama kwetu, ndiyo huo mwendo wetu,
Ligi ni timu mbili tu, kupata makombe yetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

10.Marekani sio kwetu, hali zao ziko kwatu,
Mefanya mambo kiutu, kuweka tuvituvitu,
Timu zote mambo kwatu, kuzidiana si kitu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

11.Mishahara siyo yetu, ukubwa huo si kitu,
Ila wamefanya kitu, yote yakaa kiutu,
Kupandisha hovyo katu, pita ukomo thubutu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

12.Kingine kizuri kitu, mikataba minono tu,
Runinga kuonesha tu, gawa pasu kwa pasu tu,
Kwa Uingereza katu, sijajua hapa kwetu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

13.Washindi huko si kwetu, wanabadilishana tu,
Hakuna mwenye kiatu, na mwingine yuko butu,
Ligi zao ziko kwatu, ni ujanjaujanja tu,
Kwa huku tunakokwenda, tuuchague mfumo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news