NDANI YA KOKWA LA EMBE- 2: Mwaka huu mwaka dume…

NA LWAGA MWAMBANDE

UKITAZAMA msimamo wa Ligi Kuu ya Soka ya NBC Tanzania Bara utabaini kuwa,kila timu msimu huu imedhamiria kuwashangaza mashabiki wa soka Tanzania.

Sababu kuu, inachagizwa na namna ambavyo timu au klabu hizo zinavyoonesha ubora wake. Viongozi wake wamewasaka wachezaji bora kutoka ndani na nje ya Tanzania, vijana baada ya kupewa kandarasi na maelekezo ya nini wakifanye, wala hawafanyi mizaha.

Matokeo yake, ushindani umeendelea kuwa mkubwa, kwa sasa hauwezi kushangaa vigogo wa soka Tanzania, wakitoka droo au kufungwa na timu changa ya juzi, kutokana na ukweli kwamba, uwekezaji wa maana umefanyika. Ungana na mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande akujuze kitu kupitia sehemu hii ya pili ya shairi hapa chini;

1.Mwaka huu mwaka dume, timu ziko bora hasa,
Zimesajili waume, ligi waijua hasa,
Si ajabu wasimame, vigogo kuvitikisa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

2.Azam nairudia, kweli iko bora hasa,
Mwenyewe lishaingia, usajili hakukosa,
Mambo wametufanyia, ni kandanda ya kisasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

3.Singida Big Stazi, wanakonga nyoyo hasa,
Uwanjani kazi kazi, wanatumia fursa,
Wachezaji viongozi, ubingwa lishaunasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

4.Wakigeni wahesheni, tena waupiga hasa,
Na wenyeji si wageni, ligi walishatikisa,
Mambo mazuri njiani, yanakuja tutanasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

5. Mechi chache wamecheza, mpira siyo anasa,
Wenyeji wawakimbiza, kila mpya ukurasa,
Kipimo tunakiwaza, kwa hawa wa Bongo hasa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

6.Ilivyokuwa zamani, kusajili nje hasa,
Ni timu tatu nchini, zile zilitamba hasa,
Zingine likuwa duni, sababu kubwa ni pesa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

7.Hivi utaenda wapi, siwakute hao sasa,
Nitajie timu ipi, iliyofanya makosa?
Zote zimekwishakopi, sajili zao zagusa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

8.Nenda kaanze Kagera, ona wanavyotikisa,
Namungo kiuza sura, waweza kukunyanyasa,
Ihefu nao ni bora, japo ushindi wakosa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

9.Pongezi wapate wengi, kufikia hapa hasa,
Jinsi waupiga mwingi, timu zawa za kisasa,
Wadhamini wengi wengi, wanaongeza fursa,
Ndani ya kokwa la embe, dudu laweza ingia.

10.Ujeba wao vijeba, wengine wagusagusa,
Wakidhani wameshiba, mataji watayakosa,
Haba na haba kibaba, chajaa kama tutusa,
Ndani ya kokwa le embe, dudu laweza ingia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news