NHC yavutia wengi Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini Geita,waelezwa kuhusu Samia Housing Scheme (SHC)

NA DIRAMAKINI

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) linashiriki Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika karika viwanja vya Bombambili mjini Geita.
Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Bw.Daniel Kure akiwaelezea wananchi kuhusu miradi ya shirika walipotembelea banda la NHC katika maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mjini Geita Mkoa wa Geita.

NHC inashiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kuwafahamisha wananchi juu ya miradi yake mbalimbali inayotekeleza nchini.

Akizungumza na baadhi ya wananchi waliofika katika banda la NHC, Afisa Mauzo na Masoko Mwandamizi, Bw. Daniel Kure amewajulisha wananchi hao juu ya uuzaji wa nyumba za makazi zilizopo Iyumbu na mradi wa nyumba za makazi ujulikanao kama Samia Housing Scheme (SHC) utakaojengwa katika eneo la Tanganyika Packers Kawe jijini Dar es Salaam.
"Ndugu zangu tuko hapa Geita kwa ajili ya kuwajuza juu ya uuzwaji wa nyumba zetu zilizoko Iyumbu Dodoma ambazo tunaziuza kwenu wananchi zikiwemo za vyumba viwili kwa bei ya shilingi milioni 52 hadi shilingi milioni 56 na za vyumba vitatu kwa bei ya shilingi milioni 68 hadi shilingi milioni 73 na zote ziko tayari kwa watu kununua na tayari baadhi wamekwishahamia,"amesema Bw.Kure.

Bw.Kure ameongeza kuwa, katika mradi huo wa Iyumbu pia kuna nyumba za vyumba vitatu zenye ukubwa wa square mita 120 ambazo zinauzwa kwa bei ya shilingi milioni 83 hadi shilingi milioni 87. Ambako huko nyumba zimegawanyika katika ukubwa tofauti zikiwemo za ukubwa wa square mita 75, 100 na 120.
Akizungumzia Mradi wa Samia Housing Scheme (SHC),Bw.Kure amesema kwamba, wamekuja na fomu za maombi (booking) kwa ajili ya wananchi kujaza ili kuweza kujipatia nyumba zitakazojengwa hivi karibuni kwa ukubwa tofauti tofauti.

"SHS ni mradi mkubwa upakaokuwa na nyumba za aina tatu zikiwemo za ukubwa wa square mita 89.5 vyumba vitatu, square mita 67.7 vyumba viwili na square mita 21.2 chumba kimoja na vyumba vyote hivi vina master bedroom,"amesema Bw.Kure.
Miongoni mwa wateja, Bi.Anna Mwandesya akizungumza na Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Bw.Daniel Kure alipotembelea banda la NHC katika maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mjini Geita Mkoa wa Geita.

Aidha, baada ya Bw.Kure kutoa maelezo hayo,mmoja wa wananchi waliofika kwenye banda la NHC, Bi. Anna Mwandesya alionesha kufurahishwa na uanzishwaji wa mradi wa Samia Housing Scheme (SHC) na kusema kuwa utakuwa mkombozi kwa wananchi kwa kuwa unatoa fursa ya kila mwananchi mwenye uwezo kupata nyumba hizo.

"Kwanza niwapongeze NHC kwa kazi kubwa mnayoifanya, lakini niwaombe mtujengee na sisi hapa jengo kubwa la biashara kama ambavyo tunasikia kwa mikoa mingine mlivyojenga ili nasi mbali ya kunufaika na nyumba mlizozijenga Bombambili basi nasi wafanyabiashara tupate jengo kubwa la biashara kwa kuwa kodi zenu ni rafiki tofauti na tupakopanga kwa watu binafsi,"amesema Mwandesya.
Ameongeza kuwa, mradi ujao wa Samia Housing Scheme (SHC) kwa namna unavyoelezewa unaonekana utakuwa mradi mzuri sana na wenye kuleta tija kwa wanunuzi na Taifa kwa ujumla, kwani mpangilio wa vyumba vyake ni rafiki, "hasa chumba mnachokielezea cha studio ambacho unaweza kukipangisha na mwenye nyumba ukawa unaishi hapo hapo na hii itasaidia kupata ahueni kwa mnunuzi aliyechukua mkopo benki,"amesema.

Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) linashiriki kwa mara ya pili katika maoenesho haya ambayo kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo "Madini na Fursa za Uchumi, Ajira kwa Maendeleo Endelevu" ambapo yanatarajiwa kufikia tamati Oktoba 8, mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments