'Njooni mikoa ya Kaskazini kuna fursa lukuki za kiuchumi'

NA DIRAMAKINI

LEO Septemba 3, 2022 viongozi wa Serikali kutoka mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara wamekutanishwa katika jukwaa moja na Watch Tanzania ili kuwashirikisha Watanzania na wadau mbalimbali wa maendeleo fursa za kiuchumi zinazopatikana katika mikoa hiyo ya Kanda ya Kaskazini.
Mjadala huo ambao uliongozwa na mada iliyoangazia maendeleo na fursa za kiuchumi katika mikoa umerushwa mubashara kupitia Mtandao wa Zoom na vyombo mbalimbali vya habari kuanzia saa tano asubuhi hadi saa saba mchana, ili kuweza kufahamu kilichojiri, endelea hapa;

MHE.OMARY TEBWETA MGOMBE, MKUU WA MKOA WA TANGA

"Mheshimiwa Rais (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) baada ya kuona msongamano wa mizigo pale Bandari ya Dar es Salaam ametoa fedha bilioni 300 kwa jili ya ujenzi na ukarabati wa bandari ya Tanga na uchimbaji wa chelezo, zamani bandari ya Tanga ilipokea shehena tani laki 7 ila baada ya ujenzi inakwenda kupokea shehena tani milioni 3;
"Kupitia tozo mkoa wa Tanga umeweza kunufaika na ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Tanga kupitia Pangani, Makurunge mpaka Bagamoyo, ambapo barabara hiyo itaunganisha mikoa ya Kaskazini na Dar es Salaam na kupunguza karibu kilomita 100 za usafiri,"amesema.

MHE. JOHN WANNEY MONGELLA, MKUU WA MKOA WA ARUSHA

"Kwenye hii Awamu ya sita tumejioneatTozo zikitumika katika kuleta maendeleo kwa wananchi hapa mjini Arusha. Mfano, tumepewa bilioni 3 kwa ujenzi wa Hospitali ya Longido, bilioni 2 Hospitali ya Jiji la Arusha, bilioni 3 Hospitali ya Ngorongoro pale Loliondo na bilioni 3 Hospitali ya Karatu.
"Kupitia tozo sekta ya elimu imeweza kunufaika kwa kiasi kikubwa, Arusha tuna halmashauri saba na zote zimepewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu, hosteli na vifaa za shule kama madawati, vitabu na vitendea kazi vingine vyote, hii ni hatua kubwa sana katika nchi yetu,"amesema.

MHE. NURDIN H. BABU, MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO

"Mkoa wa Kilimanjaro una jumla ya shule za awali 961, msingi 963, sekondari 348 (katika hizi 69 ni za kidato cha tano na sita) pia ina vyuo vya ualimu 10 na vikuu 6 pamoja na vyuo vya VETA 69 ambayo vinaendeshwa na taasisi za kiserikali na sekta binafsi.

"Katika mwaka wa fedha wa 2021-2022 Mkoa wa Kilimanjaro tulipokea bilioni 6.4 kwa ajili ya uboreshwaji wa sekta ya elimu ya awali, msingi na sekondari kwenye fedha za tozo tumepewa bilioni 14 kwa ajili ya kujenga hospitali 4 mpya katika wilaya za Same, Mwanga, Manispaa ya Moshi na Moshi Vijijini,"amesema.
MHE. CHARLES M. NYERERE, MKUU WA MKOA WA MANYARA

"Uwekezaji wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo vinahitajika sana katika Mkoa wa Manyara kwani uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka ni tani 489,379 na tani za biashara ni laki 137,659 hivyo ujenzi wa viwanda hivi vitakwenda kuongeza thamani ya mazao yapatiakanyo mkoa wa Manyara.
"Mkoa wa Manyara una fursa nyingi sana mfano kwenye kilimo, mkoa una hekta zaidi ya milioni 1.5 lakini zinazotumika ni hekta laki 8 sawa na asilimia 54 na ambazo zinafaa kwa ajili ya umwagiliaji ni hekta 29,000 huku mazao yanayolimwa ni ya chakula kama mahindi, mihogo, ulezi, ngano na mazao ya biashara ni miwa, alzeti, pamba, kahawa, ngano n.k.

DISMAS PROSPER, MENEJA WA KANDA YA KASKAZINI NMB

"Benki ya NMB tayari imeshatoa shillingi bilioni 3 kwa ajili ya wakulima wa zao la mihogo kule Handeni, ikiwa ni jitihada ya kuwezesha zao hilo la kibiashara kupanda thamani, pia katika mkoa wa Tanga tumetoa shillingi bilioni 6 kwa wakulima wa zao la mkonge.
"Kiujumla nchi nzima tumeshatoa mikopo ya shillingi trilioni 1.2 kwenye mnyororo wa kilimo, uvuvi na ufugaji, hii ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta matokeo chanya katika sekta ya kilimo na sekta ya ufugaji nchini,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news