Serikali yatoa maagizo ucheleweshaji hati za ardhi; changamoto yoyote piga 0739646885 au 026216110

NA DIRAMAKINI

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema kuwa, imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kucheleweshwa kupatiwa hati, hata baada ya kukamilisha taratibu zinazokidhi vigezo.

Kufuatia hali hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Dkt.Alan Kijazi ameelekeza ofisi zote za Ardhi za Mikoa kuhakikisha zinakamilisha zoezi la utoaji hati kwa zile hati ambazo taratibu zake zimekamilika ndani ya mwezi mmoja kuanzia tarehe ya tangazo hili leo Septemba 21, 2022.

"Aidha, kama kuna kikwazo chochote cha utoaji hati kwa sababu yoyote ile,wahusika watapewa taarifa ya maandishi ya sababu ya hati kuchelewa na kushauriwa hatua za kuchukua ili taratibu zikamilishwe.

"Pamoja na taarifa hii, Wizara ya Ardhi inapenda kuufahamisha umma kuwa, ofisi zote za Ardhi za Mikoa zimeanzisha utaratibu wa kutoa huduma jumuishi za utoaji hati (One Stop Office) kwa lengo la kurahisisha upatikanaji Hatimiliki
za Ardhi.

"Utaratibu huu unalenga kuondoa usumbufu wa kufuatilia taarifa za kukamilisha hatua mbalimbali za kisheria kabla ya kupata hati,"imefafanua sehemu ya taarifa iliyotolewa leo Septemba 21, 2022 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wizara pia inapenda kuwafahamisha wamiliki wote wa ardhi kuwa, inazo takribani Hati 20,000 zilizokamilika lakini wahusika hawajazichukua.

"Wito unatolewa kwa wahusika wote kufika ofisi za Ardhi za mikoa kuchukua hati zao. Orodha za Hatimiliki ambazo hazijachukuliwa zimebandikwa katika mbao za matangazo za Ofisi za Ardhi za Mikoa na Halmashauri nchini.

"Aidha, Wizara ya Ardhi inamtaka mwananchi yeyote mwenye malalamiko ama changamoto kuhusu utoaji huduma za sekta ya ardhi kwenye ofisi zetu kupiga simu Kituo chetu cha Huduma kwa Wateja kupitia simu 0739646885 au
026216110 kwa ajili ya kuwasilisha kero yake,"imefafanua taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news