Watoto 263,990 kupatiwa chanjo ya polio Pwani

NA ROTARY HAULE

KAMPENI ya chanjo ya polio imeanza kutolewa leo Septemba 1,2022 katika maeneo tofauti hapa nchini ambapo Mkoa wa Pwani unatarajia kuchanja zaidi ya watoto 263,990.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt.Gunini Kamba amewaambia waandishi wa habari leo ofisini kwake kuwa, kampeni hiyo itafanyika kwa muda wa siku nne kuanzia Septemba 1 hadi 4, mwaka huu.

Dkt.Gunini amesema kuwa, kampeni hiyo inafanyika kwa awamu ya tatu ambapo lengo lake ni kuwafikia watoto wote waliopo Mkoa wa Pwani wenye umri chini ya miaka mitano.

Amesema,katika kufikia malengo hayo mkoa umeweka mkakati wa kuhakikisha timu ya uchanjaji inapita nyumba kwa nyumba,sokoni,shule za chekechea na nyumba za ibada.

"Ni muhimu kila mtoto apate chanjo hii ili kuimarisha kinga yake na kuzuia ugonjwa usiingie nchini ,chanjo ni zawadi ya maisha kwa mtoto,hivyo sote inatupaswa tuelewe kuwa jamii iliyochanjwa ni jamii yenye afya bora kwa maendeleo ya Taifa,"amesema Dkt.Kamba.

Aidha,Dkt.Kamba amesema kuwa, watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano bila kujali kama walipata chanjo hiyo wanapaswa kuchanjwa kwa kuwa itaongeza kinga katika mwili.

Amesema kuwa,mkoa ulifanya vizuri katika chanjo ya awamu ya pili kwa kuwa ulivuka lengo la uchanjaji kwa asilimia 131 ya walengwa wote na kwamba matarajio ni kufanya vizuri zaidi katika awamu hii ya tatu.

"Awamu ya pili ya chanjo hii ya polio Mkoa wa Pwani tulichanja watoto 263,851 lakini katika awamu hii malengo ni kuchanja watoto 263,990 waliopo katika Mkoa wa Pwani,"amesema Dkt.Kamba.

Amesema,ugonjwa wa Polio unasababishwa na kirusi cha Polio ambacho huambukizwa kutoka kwa mtu aliyeathirika kwenda kwa mtu mwingine kwa kunywa au kula chakula au kinywaji kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea vya ugonjwa wa Polio.

"Virusi vya Polio huzaliana katika utumbo na huweza kuathiri mfumo wa fahamu ikiwa ni pamoja na kuathiri mfumo wa neva hivyo kupelekea kupooza kwa ghafla kwa viungo ndani ya masaa machache na hata kupelekea kifo na ugonjwa huu huathiri zaidi watoto chini ya miaka kumi na mitano,"ameongeza Dkt.Kamba.

Kamba,ametoa wito kwa viongozi na watendaji wote wa Serikali,vyama vya siasa,dini,taasisi,wazazi na wadau wote wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha wanashiriki kikamilifu juu ya zoezi hilo.

Kwa upande wake mratibu wa chanjo Mkoa wa Pwani, Abbas Hincha amesema kuwa , chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote na imekuwa kawaida kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kupata chanjo hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news