ALAMA BARABARANI-5:Kuzifwata kunalipa, ajali hatutaona

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, alama za barabarani zina umuhimu mkubwa sana, alama hizo huwa zinatoa maelekezo na pia kuonya ili kuhakikisha watumiaji wa barabara wanakuwa salama muda wote.

Aidha,upuuzaji wa alama za barabarani mara kwa mara husababisha ajali za barabarani. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,kila mmoja wetu analo jukumu la kuzitilia maanani na kuziheshimu alama hizo kwa usalama wako na watumiaji wengine wa barabara, endelea;

1:Alama barabarani, hizi ni muhimu sana,
Kama tukiwa makini, zote zikaonekana,
Nasi tukiwa njiani, na hizo kuambatana,
Ajali tuzipatazo, zaweza zikapunguka.

2:Nitataja chache hapa, ambazo mnaziona,
Kuzifwata kunalipa, ajali hatutaona,
Zipo siyo za kukopa, ni nyingi tunaziona,
Ajali tuzipatazo, zaweza zikapunguka.

3:Za kwanza zile za mwendo, ambazo tunaziona,
Kuna huru wa mwendo, hapo tunakimbizana,
Na za kudhibiti mwendo, kuzidi hapo hapana,
Ajali tuzipatazo, zaweza zikapunguka.

4:Kimbia kwa thelathini, vibao tunaviona,
Usizidi hamsini, ni vingi tunakutana,
Kama tukiwa makini, ajali hatutaona,
Ajali tuzipatazo, zaweza zikapunguka.

5:Ukae barabarani, magari utayaona,
Kwa madereva makini, alama wanaziona,
Wale wasio makini, mwendo wao utaona,
Ajali tuzipatazo, zaweza zikapunguka.

6:Kama tukii sote, bila hata kubishana,
Na tukipendana sote, pasi hata kupishana,
Ajali zingine zote, kwa kwendo hatutaona,
Ajali tuzipatazo, zaweza zikapunguka.

7:Alama pia muhimu, mimi vile ninaona,
Mistari ni adhimu, ambayo tunaiona,
Madereva wafahamu, tena waipenda sana,
Ajali tuzipatazo, zaweza zikapunguka.

8:Inatenga barabara, pande mbili twaziona,
Hapo hakuna madhara, kuweza ingiliana,
Hata giza si hasara, ambayo waweza ona,
Ajali tuzipatazo, zaweza zikapunguka.

9:Mingine ya pembezoni, ya njano tunaiona,
Inatufanya makini, hata tukipiga kona,
Tusiende korongoni, ajali zikatubana,
Ajali tuzipatazo, zaweza zikapunguka.

10:Tunaomba mamlaka, hizi alama kuona,
Zile zilizofutika, ili kuzichora tena,
Tusijikute mateka, njiani tukagongana,
Ajali tuzipatazo, zaweza zikapunguka.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments