Waziri Simbachawene aita wananchi kuwekeza Dodoma

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene ametoa wito kwa jamii kuwekeza Dodoma kwa kuzingatia fursa zilizopo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuendeleza jiji hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe.George Simbachawene pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakitembelea na kukagua jengo la Ofisi ya Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwa ni sehemu ya ziara yao katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma.

Ametoa kauli hiyo Oktoba 24, 2022 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipotembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Akieleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri Simbachawene amesema ofisi yake ina jukumu la kuratibu na kusimamia mradi wa ujenzi wa majengo ya wizara na taasisi zake, hivyo atahakikisha ujenzi huo unasimamiwa kwa weledi na kukamilika kwa wakati.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. George Simbachawene pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakiangalia muonekano wa juu katika moja ya chumba cha jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii wakati wa ziara hiyo.

“Hadi sasa ujenzi umefika asilimia 50 hadi 80 kwa baadhi ya majengo na kwa upande wa miundombinu ya barabara, nishati, maji na mawassiliano ipo vizuri hivyo nitoe rai kwa wananchi kutumia fursa zilizopo ili kuwekeza Dodoma,"amesema Waziri Simbachawene.

Ameongezea kuwa, uwepo wa mji wa Serikali itasaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa wepesi zaidi.
Mjumbe wa kikosi kazi cha kuratibu Ujenzi wa Mji wa Serikali, Bw.Noel Mlindwa akitoa maelezo kuhusu hatua zilizofikia katika ujenzi huo wa majengo ya ofisi za wizara katika Mji wa Serikali, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria jijini Dodoma.

"Mji huu ndiyo utafanikisha na kurahisisha shughuli za Serikali kwa urahisi kwani kila wizara itakuwa hapa na itafikika kwa wepesi, na niwakaribiahe wananchi kuja kupata huduma mahali hapa,"amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt.Joseph Mhagama aliipongeza Serikali ya Awamu wa Sita kwa namna inavyowezesha ujenzi wa Mji wa Serikali kwenda kwa kasi na hii inafaa kuungwa mkono.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe Dkt. Joseph Mhagama akizungumza mara baada ya kujionea na kujiridhisha maendeleo ya Mji huo.

"Ninampongeza Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza Mji huu, na Kamati imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi hivyo ninawapongeza ofisi ya Waziri Mkuu kwa kufanya kazi kwa weledi,”amesema Dkt. Mhagama.

Akitoa neno mjumbe wa kamati hiyo Mhe.Asha Abdallah ametoa kongole kwa kazi kubwa inayofanywa na serikali huku akiwaasa watanzania kutumia mji huo katika kupata huduma kwakuwa unafikika kwa wepesi.
Waziri Wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene akizungumza wakati wa majumuisho mara baada ya ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo katika Mji wa Serikali eneo la Mtumba Jijini Dodoma tarehe 24 Oktoba, 2022.

"Ofisi hizi kupatikana mahali pamoja ni jambo nyeti litakalopunguza kero kubwa za wananchi kwani wizara zote zitafikika kwa wepesi, jueni kuwa serikali haijawatupa inajali sana,"amesema.

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Salum Shafi amesema kila mmoja aone umuhimu wa kulinda na kutunza majengo yatakayotumika na kuhakikisha wanakuwa wazalendo.
Waziri Wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria mara baada ya kuhitimisha ziara yao katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU).

"Mradi huu ni fedha za walipa kodi, hivyo kila mmoja awe mzalendo katika kutunza na kulinda yaweze kutumika kwa muda mrefu katika ubora wake na kuongeza tija katika shughuli za Serikali ,hakika Dodoma imepambika na mama ameifanya kazi vizuri mama tunakupongeza,”alisisitiza.

Post a Comment

0 Comments