Balozi Boer ataja faida za uhuru wa vyombo vya habari

NA DIRAMAKINI

BALOZI wa Uholanzi nchini Tanzania, Mheshimiwa Wiebe de Boer amesema,uhuru wa vyombo vya habari ni miongoni mwa nguzo muhimu katika kuchochea ukuaji wa maendeleo kiuchumi na ustawi bora wa demokrasia.

"Uhuru wa habari ni nguzo muhimu katika ustawi wa demokrasia na kuchochea maendeleo ya taifa.Demokrasia kamilifu inategemea upatikanaji wa taarifa kwa uwazi na za kuaminika.

"Vivyo hivyo, ustawi wa maendeleo unategemea taarifa sahihi na za kuaminika, hivyo nichukue nafasi hii kuipongeza TEF kwa kushiriki kikamilifu katika kutoa hamasa na elimu juu ya umuhimu wa maboresho ya sheria za habari nchini.

"Na tumeona juhudi kubwa ambazo zinafanywa na Serikali, Rais (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) ameonesha dhamira njema katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, nasi tutaendelea kuunga mkono juhudi hizo;

Mheshimiwa Balozi Boer ameyasema hayo leo Oktoba 20, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo maalum ya siku moja kwa wahariri na wanahabari yanayoangazia uchechemuzi wa sheria za vyombo vya habari nchini ambayo yanaratibiwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Licha ya kufurahishwa na ujumuishwaji mkubwa wa wanawake katika mafunzo hayo, Balozi Boer amewataka wanahabari kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha mazingira wezeshi ya upatikanaji wa habari nchini.

Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeonesha dhamira njema ya kuzifanyia maboresho sheria za habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kubinya uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha, Rais Samia alitoa maagizo;

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,”aliagiza Rais Samia.

Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Salim Salim amesema, Rais Samia ana dhamira njema na tasnia ya habari, lakini changamoto mara nyingi huwa ni kwa baadhi ya watendaji ambao utekelezaji wa majukumu yao, huwa hauendani na kasi ya mkuu wa nchi.

"Tunathamini na kuheshimu sana maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhusu maboresho sekta ya habari, lakini tunashauri maagizo hayo yaendane na uundwaji wa sheria na kanuni kwa haraka ili vyombo vya habari nchini viendelee kuheshimiwa,"amesema Mzee Salim.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Bw. Deodatus Balile amesema,kwa sasa mwamko wa uhamasishaji wa mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari umeongezeka na umetoa matokeo mazuri na wanaendelea kuishukuru Serikali kwa kuonesha utayari wa kufanya maboresho.

"Lazima tuwe na moyo wa shukurani kwa Serikali, tumeona magazeti ya Mawio, Tanzania Daima na Mseto yakifunguliwa na kuna juhudi mbalimbali zinaendelea ili kuhakikisha sheria ambazo zinaonekana kubinya uhuru wa vyombo vya habari zinafanyiwa maboresho,"amebainisha.

Agosti 26, 2022 Serikali kupitia Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliwahakikishia wadau wa habari kuwa, Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Habari nchini hayatapelekwa bungeni bila pande zote kukubaliana na kuridhika.

Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye aliyasema hayo katika mjadala wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC ambao uliangazia kuhusu mapendekezo hayo.

"Nimeletewa ripoti ya majadiliano yale, tunakwenda hatua ya pili sasa kule ambako walishindwa kukubaliana, tunataka tuongeze kikao kingine tukajadili yale tu ambayo hatukukubaliana.

"Lakini, niwahakikishie wadau wa habari kwamba, hatutaenda bungeni bila kukubaliana,lazima tukae tukubaliane, tushauriane tufikie mwisho.

"Hatutaki kutunga sheria kesho na kesho kutwa tukarudi tena kwenda kurekebisha, na ndiyo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwamba tukae tuzungumze, tujadiliane mpaka tukubaliane.

"Kwa hiyo tutakwenda, tutazungumza. Na mimi nina hakika kwamba tutakubaliana na spirit iliyopo ni nzuri, Serikali tupo tayari kuondoa baadhi ya vifungu, kwa sababu hatuna nia mbaya.Lakini pia Jukwaa la Wahariri na wadau wa habari kwa spirit ambayo ninaiona wapo pia tayari kukubaliana baadhi ya mambo. Kwa hiyo twende tukashawishiane,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Nape.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news