BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 45

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...lengo letu lilikuwa ni kutua eneo la ujenzi wa GAMBOSHI MPYA, pale tungeshuka kwa ajili ya kumchinja mbunge huyo kama kafara. Lakini ilishindikana hivyo tukaenda kutua kwenye kambi yetu kuu tukiwa na yule kafara.

Endelea.

Tulishuka kambini hapo tukiwa salama bin salimini, walikuja kutupokea baadhi ya wachawi wenzetu. Hivyo niliwakabidhi yule kafara kisha wakampeleka eneo maalumu, eneo hilo lilikuwa likitumika kuhifadhia kafara wa aina mbalimbali.
THE BOMBOM nikaamua kuelekea kwenye jengo kuu la utawala, katika jengo hilo ndimo yalikuwa makazi ya viongozi wakuu wa kambi hii.

Kutoka eneo nililokuwa nimesimama, kwenda kwenye jengo hilo la utawala kulikuwa na umbali kidogo.

Ndugu msomaji, kambi ya Majengo ilikuwa ni miongoni mwa kambi kubwa ya kichawi ukanda wa ziwa Magharibi. Kambi zingine kubwa za zilikuwa eneo la Kazuramimba, Kalya, Kibondo na Kasulu.

Katika kambi hii hakuna kilichokosekana, huduma zote za kijamii zilipatikana. Tatizo la kambi hii lilikuwa kwenye majengo, kwa ujumla miundombinu ya kambi hii ilikuwa ya kizamani.

Mpangilio wake haukuwa rafiki japo kwa kipindi cha nyuma ilionekana kuwa bora. Hii ndiyo sababu mojawapo iliyomfanya mkuu wetu kutuhamasisha ujenzi wa kambi nyingine yaani GAMBOSHI MPYA.

Kwa kuwa siku hiyo hatukuwa na shughuli nyingi, misukule walikuwa wamelala kwenye majumba yao. Walioonekana kuwa na hekaheka kipindi hicho walikuwa wachawi wenzangu, yote hii ilikuwa ni maandalizi ya ujenzi wa GAMBOSHI MPYA.

Nikiwa natembea kuelekea makao makuu ya kambi, moyoni nilikuwa nikiwawaza juu ya wachawi waliosababisha tusitue kwenye eneo la ujenzi wa GAMBOSHI MPYA.

Kwa kuwa tayari nilikuwa nimeshaweka mazindiko mazito, niliamini kambi ilikuwa salama. Kwa mbali nilimuona BUNDI WA GAMBOSHI akiwa amesimama chini ya mti wa mlongelonge karibu na makao makuu ya kambi.

Alionekana kutokuwa na furaha hata kidogo, nilikwenda mahali alipokuwa bundi huyo. Nilipomkaribia nilibaini alikuwa akitokwa machozi machoni mwake, haikuwa ishara njema kwa bundi huyo.

Ilikuwa ni ishara ya mambo kutokwenda sawa kambini hapo ama kule kwenye ujenzi wa GAMBOSHI MPYA.

Ghafla bundi huyo alitikisa mbawa zake, zake ikadondoka chupa ndogo karibu yangu. Alijitikisa mara ya pili ikadondoka karatasi iliyokuwa imefungwa vitu kwa ndani yake, niliichukua pia karatasi hiyo.

Kwa kuwa hili halikuwa geni machoni mwangu, nilifungua chupa hiyo ndogo kisha nikamimina kilichomo ndani yake kiganjani mwangu.

Ilikuwa ni dawa yenye rangi nyekundu nikaipaka mwili mzima. Baada ya hapo nilifungua pia ile karatasi, kulikuwa na dawa yenye rangi nyeusi nikajipaka machoni, miguuni na mikononi kama nilivyoelezwa na BUNDI WA GAMBOSHI.

Yule bundi alitanua vidole vyake vya miguuni na kufanya uvungu mkubwa, niliingia uvunguni humo kisha akakunja vidole vyake harafu akaruka hewani.

Hakuna mchawi aliyebaini safari hiyo kambini kwangu, punde si punde tulitua kwenye paa la jengo la shule ya msingi Airport.

Shule hiyo ilikuwa karibu sana na eneo la ujenzi wa GAMBOSHI MPYA. Sikuamini nilichokiona machoni mwangu, kulikuwa na kundi kubwa la wachawi waliokuwa wamezagaa eneo hilo wakifanya mambo yao.

Mbaya zaidi wachawi hao walikuwa hawatuoni, nikagundua kuwa ile dawa niliyojipaka ilikuwa na nguvu ya ziada.

Nilikuwa nimehifadhi ndani ya kaniki niliyokuwa nimevaa, mara BUNDI WA GAMBOSHI alipaa hewani na kwenda kutua kwenye eneo hilo kisha nikatoka kwenye uvungu wa vidole vyake.

Kulikuwa na kundi kubwa la wachawi eneo hilo, wapo niliowatambua na wengine sikuwatambua. Miongoni mwa wachawi niliwabaini, alikuwepo mchungaji wa kanisa la WISDOM OF GOD.

Huyu alikuwa ni mzungu aliyekuwa akifanyia shughuli zake za kichungaji eneo hili. Wahenga walisema umzaniaye ndiye kumbe siye, mzungu huyu alikuwa kiunganishi baina yake na wachawi wa Ulaya.

Kulikuwa na wachawi wa aina mbalimbali, walikuwepo waarabu na wahindi, hawa nilijua kabisa walikuwa wameletwa kwa kazi maalumu tena kwa gharama kubwa.

Lengo kubwa lilikuwa ni kutengua mazindiko ya ujenzi wa GAMBOSHI MPYA. Nilimuona pia Padri Jonasi Chambilacho Mzungu akiwa na wenzake, alikuwepo pia Amiri Othman Ally kiongozi mkubwa wa imani ya kiislamu kwa wilaya hii.

Kulikuwepo watu mbalimbali wengine walikuwa wageni machoni mwangu. Kazi pekee kubwa waliyokuwa wakifanya ni kutegua mazindiko yote tuliyokuwa tumeyaweka mahali hapo.

Mchungaji wa kanisa la WISDOM OF GOD, Padri Jonasi Chambilacho, Amiri Othman Ally na baadhi ya vikongwe walikuwa wakimwaga dawa kwenye misingi ya majengo yetu.

Niliwasogelea nikabadilisha dawa zao kisha nikawapatia mchanga, hawakuweza kutambua mchezo huu kwa kuwa nilikuwa nimewazidi kwa kiwango cha juu nguvu za madawa.

Kwa kiasi kikubwa dawa tulizokuwa tukizitumia kambini kwetu, asili yake ilikuwa ni kutoka Heaven. Makao makuu ya mkuu wetu japo wengine humfananisha na shetani wakati ni viongozi wawili tofauti wanaofanya kazi za kufanana.

Waliendelea kumwaga dawa zao wakijua walikuwa wakitumaliza kumbe tayari tulikuwa tumewabadilishia kibao.

Kulikuwa na kundi kubwa la wachawi waliokuwa wakipinga ujenzi wa GAMBOSHI MPYA, kwa kuwa walijua hatari ya kambi hiyo kujengwa eneo hilo. Hiki kilikuwa ni kiashiria tosha kabisa cha kupotea kwa kambi zao, ndiyo maana walipambana kwa udi na uvumba kukwamisha ujenzi wa kambi hiyo.

Kwa kuwa ilikuwa usiku mnene, taratibu wachawi walianza kusambaa huku wakirudi makwao. Kwa kiasi kikubwa wachawi wengi huwa wanarudi majumbani kabla ya kuku kuanza kuwika.

Waliendelea kutawanyika huku wakitumia usafiri wao, wapo waliotumia fisi, nyungo, upepo nk. Baada ya hapo BUNDI WA GAMBOSHI alinichukua kisha akanirudisha kambini kwetu.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji kwa hali ya kawaida ilikuwa ni vigumu kwa mtu wa kawaida kujua vita iliyokuwa ikiendelea.

Vita hii ilikuwa ikihusisha mbinu za madawa, ni watu wenye nguvu za madawa pekee ambao wangebaini vita hii.

Watu wengi wanaoheshimika ndani ya jamii wengine ni wachawi, tazama Padri Jonasi alivyokuwa akiheshimiwa na jamii ya waamini wa madhehebu yake.

Mapadri baadhi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya hovyo ndani ya jamii, wapo wanaolawiti vijana kwenye nyumba hizo za ibada.

Wengine wanawabaka mabinti na watoto wetu, wengine wanajihusisha na biashara haramu za viungo vya binadamu.

Baadhi ni wachawi mfano mzuri ni huyu Padri Jonasi Chambilacho. Unapaswa kuwa makini na watumishi hao, mara nyingi mnawatambua kwa sura moja sura ya pili hamuwatambui.

Angalia mchungaji mkuu wa kanisa la WISDOM OF GOD na Amiri Othman Ally kwa sura ya nje walionekana kuwa watakatifu kumbe la hasha!.

Ndugu msomaji mambo yameiva, kambi nyingi za wachawi zimeungana kukwamisha ujenzi wa GAMBOSHI MPYA, bahati nzuri THE BOMBOM ameling'amua hilo. Je, nini kinafuata? Tafadhali ungana na mimi katika simulizi ya sehemu inayofuata.

BHUKEBHUKE
THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news