BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 46

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia..tuliendelea na maandalizi mpaka ilipofika saa kumi na mbili jioni. Niliwaita wasaidizi wachache kwa ajili ya kupanga mipango ya namna ya kuvamia kwenye kambi ya kichawi ya Padri Jonasi Chambilacho Muzungu.

Endelea...

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji kambi zote za wachawi huwa zimezindikwa. Mazindiko ambayo huwa yamewekwa katika kambi hizo, hutofautiana toka kambi moja kwenda nyingine.

Lengo kuu la mazindiko hayo ni kuilinda kambi dhidi ya wachawi wengine. Ni jambo la kawaida sana kwa wachawi kujaribiana kwa madawa, endapo kambi itakuwa rahisi kwa mchawi yeyote kuingia huleta madhara makubwa.

Mchawi yeyote anapotaka kwenda kwenye kambi ya wachawi wengine, lazima aruhusiwe na wachawi wa kambi hiyo au afuate taratibu za kambi hiyo.

Kwa kuwa THE BOMBOM na kundi langu tulikuwa tumedhamiria kwenda kambini hapo kwa njia ya shari, tulijiandaa kisharishari.

Hatukutaka ruhusa toka kwenye uongozi wa kambi hiyo. Njia pekee ya kuingia kambini hapo ilikuwa ni kuchunguza nguvu za kambi hiyo. Tulichukua dawa ya ngabo tukachanganya na dawa ya wintororo kisha tukapaka kwenye kioo kikubwa kilichokuwa mbele yetu.

Ghafla kwenye kioo kile ilitokea video ya kambi nzima ya Padri Jonasi Chambilacho Muzungu.

Badala ya kwenda eneo husika, tuliamua kuichunguza ikiwa kwenye kioo. Mpaka hapo tulikuwa tumeihamisha kambi hiyo kutoka eneo husika mpaka chumbani kwetu.

Video ile ilikuwa ikionesha kila kitu kinachoendelea kambini hapo. Kwa kutumia video hiyo tuliweza kubaini makao makuu ya kambi hiyo. Kulikuwa na majengo mengine makubwa ambayo sikuyaacha kipindi nikiwa msukule kambini hapo.

Tukachukua dawa ya inkende tukamwaga tena kwenye kioo, dawa hii imetokana na damu na moyo wa ngedere pamoja na mizizi ya mti wa mzorwa mwekundu.

Kazi ya dawa hii ni kuonesha sehemu zote zilizowekwa zindiko, hivyo tukiwa chumbani humo tulianza kuchunguza zindiko za kambi hiyo.

Tukiwa kwenye heka heka hizo, ghafla kile kioo kiliripuka mfano wa fataki. Kilisambaratika chumbani humo huku baadhi ya wasaidizi wangu wakichomwa na vipande hivyo vya kioo.

Mlipuko huo ulitutisha sana tukabaini kuwa kambi hiyo ilikuwa imara zaidi hivyo katika kuichunguza tulitakiwa tutumie dawa imara.

Tulileta kioo kingine kikubwa na kukiweka mbele yetu, baada ya hapo tulichukua msukule mmoja tukamchinja kisha tukakinga damu yake.

Tulichukua dawa nyingine iitwayo bwanda, dawa hii ni mchanganyo wa kivuli cha jini na sanda ya maiti aliyezikwa mjamzito.

Tukachanganya na dawa ya mososa na ile damu ya msukule kisha tukavimwaga juu ya kioo kile, baada ya muda kile kioo kilileta video nyingine kubwa ya kambi hiyo ya Padri Jonasi Chambilacho Muzungu.

Tuliendelea kuichunguza kambi hiyo huku tukitengua zindiko zote, hatimaye tulifanikiwa kutengua zindiko kwenye kambi hiyo huku tukiwa chumbani kwetu. Kazi hiyo tuliikamilisha muda wa saa moja jioni, wakati huo tulikuwa na uhakika wa kuingia kambini hapo bila kikwazo chochote.

Niliwaruhusu wasaidizi wangu kwenda kujiandaa kwa safari hiyo ya usiku, safari ilikuwa ngumu lakini tulipaswa kuikamilisha kwa namna yeyote. Niliingia chumbani kwangu nikajipunzisha kidogo, kichwani nilijawa furaha ya kulipa kisasi dhidi ya wazazi wangu pamoja na Padri Jonasi Chambilacho Muzungu.

Saa nne za usiku tulikutana kambini kwetu tayari kwa safari, nilikuwa na wachawi wenzangu kumi na moja.

Tulichukua vifaa vyetu kisha tukapanda ndani ya usafiri wa ungo tukaondoka. Tulikwenda kutua mji wa Musoma karibu na kambi hiyo, tukaamua kutembea kwa miguu tukiwa kwenye maumbo yetu.

Kambi hiyo ilikuwa pembeni mwa daraja la mto Malagarasi. Kwa macho ya kawaida ni vigumu kuiona, labda uwe na macho ya roho yanayoshirikisha madawa makali.

Ni mji mkubwa zaidi ya mji halisia wa Musoma uliopo eneo hilo, kuna majengo makubwa yaliyozunguka eneo hilo. Kuna barabara nzuri zinazotoka eneo hilo mpaka mji wa Musoma, kuna umeme wa kutosha pamoja na maji.

Kulikuwa na idadi kubwa ya misukule waliokuwa wakifanya shughuli mbalimbali kama walivyokuwa wamepangiwa.

Tulisimama mbali kidogo na kambi hiyo kisha tukachukua dawa ya Ngw'acha tukaichanganya na dawa zingine akatokea kiumbe mfano wa ndege mdogo.

Tukamtuma ndege huyo kuingia kambini hapo. Japo tulikuwa tumeondoa zindiko la kambi hilo, hatukupaswa kuingia kichwa kichwa. Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji kuna kipindi unaweza kuona ndege mweusi tii au mweupe pee batini kwako nashauri uwe makini.

Ndege wa aina hii huwa wametulia sana huku wakionekana kama wanasinzia. Hawa siyo ndege wa kawaida, ni ndege wa madawa ambao huwa tunawatumia kuchunguza mambo kadha wa kadha kwenye eneo lililokusudiwa.

Baada ya muda kidogo yule ndege alirudi akiwa salama kabisa, nikamuagiza mchawi mmoja kwenda kambini hapo. Alikwenda kama nilivyokuwa nimemuagiza, baada ya dakika chache alirudi akiwa salama.

Nikaendelea kuwatuma wasaidizi wangu mmoja baada ya mmoja, walikwenda na kurudi salama. Hapa ndipo nikaamini kuwa tulikuwa tumefanikiwa kutengua mazindiko ya kambi hiyo.

Tukaingia kwenye kambi hiyo kibabe, tukamwaga dawa kambi nzima pasipo wao kutuona. Tulikwenda mpaka kwenye jengo la makao makuu ya kambi, kule tuliwakuta Padri Jonasi Chambilacho Muzungu na kundi lake wakiwa kwenye kikao.

Tukamwaga dawa ya kuwazuia kutoka eneo hilo, kisha tukaendelea kumwaga dawa eneo jingine kambini hapo.

Moyoni nilijawa kinyongo juu ya mambo mabaya walionifanyia wazazi wangu, bahati mbaya siku hiyo alikuwepo baba tu.

Mama yangu mzazi hakuwepo kwenye kikao hicho, nilitamani sana kulipa kisasi kwao maana walishirikiana kunifanya msukule.

Mara nyingi wanawake huwa na huruma kwa watoto wao wa kuzaa, lakini ilikuwa tofauti kabisa kwa mama yangu mzazi. Yeye alitokea kunichukia toka nilivyomuokoa Ndolimana mikono mwa wachawi.

Mambo ndiyo yameiva,THE BOMBOM tayari yupo kwenye kambi ya Padri Jonasi Chambilacho Muzungu. Je, atafanikiwa kulipa kisasi? Naomba uungane na mimi katika sehemu inayofuata.

WABONYE
THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news