DC Mkasaba:Serikali itaendelea kushirikiana na SOS kuwaenzi na kuwatunza watoto

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha zinaunga mkono juhudi na mikakati ya kuwaenzi na kuwatunza watoto zinazochukuliwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Vijiji vya Watoto nchini (SOS Tanzania).
Mkuu wa Wilaya ya Kusini Rajab Yussuf Mkasaba ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya Kikanda ya Kujadili Mradi wa kuwaunganisha watoto wa vijiji vya SOS kwenye familia zao za asili yaliyofanyika huko katika hoteli ya Visitors Inn Jambiani Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika hotuba yake Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini amesema kuwa, hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi na mikakati inayochukuliwa na Serikali zote mbili hapa nchini katika kuhakikisha watoto wote wanapata haki zao za msingi.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini,Mheshimiwa Rajab Yusuf Mkasaba akifurahia jambo na mshiriki wa mafunzo, Bi.Lene Godiksen kutoka nchini Dernmark.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusonio ametumia fursa hiyo kuwaeleza washiriki hao wa mafunzo hayo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini kazi kubwa inayofanywa na Kijiji cha kulelea watoto cha Zanzibar SOS na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wake katika Mradi wa kuwaunganisha watoto wa vijiji vya SOS kwenye familia zao za asili.

Ameupongeza uongozi wa vijiji vya kulelea watoto SOS kwa kuichagua Zanzibar hasa Wilaya ya Kusini na kufanya mafunzo hayo ya siku tano ambayo yalijadili masuala mbalimbali juu ya mustakbali wa watoto pamoja na haki zao za msingi katika nchi zenye vijiji vya kulelea watoto SOS.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika uongozi wao wamekuwa wakifanya juhudi za makusudi katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi, hivyo kuna kila sababu ya kuungwa mkono,”amesema Mkasaba.
Aidha, Mkasaba amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lililokusudiwa kwa nchi zenye vijiji vya kulelea watoto SOS na kuvipongeza vya kulelea watoto SOS vya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuandaa mafunzo hayo hapa nchini.

Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Wilaya amezipongeza nchi za Denmark, Norway, Austria, Finland na nyinginezo kwa kuendelea kuviunga mkono na kuvisaidia vijiji vya kulelea watoto SOS katika nchi mbalimbali za Bara la Afrika.

Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Athanas Paul amepongeza hatua hiyo ambayo amesema kwamba itasaidia kwa kkasi kikubwa kuwaenzi na kuwatunza watoto hapa nchini.

Nao washiriki wa mafunzo hayo kutoka nchi zote zenye vijiji vya kulelea watoto SOS wameeleza kwamba, juhudi za makusudi watazichukua katika kuhakikisha mafunzo waliyoyapata wanayafanyia kazi katika nchi zao.

Aidha,Naibu Waziri huyo amewahakikishia washiriki hao kwamba Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.

Pia washiriki hao wameeleza kwamba,ushirikiano wa pamoja unahitajika katika kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa ili watoto waweze kuishi kwa amani na upendo.
Washiriki kutoka nchi mbalimbali zenye vijiji vya kulelea watoto SOS walihudhuria mafunzo hayo wakiwemo kutoka nchi ya Denmark, Ghana, Ethiopia, Kenya, Malawi, Botswana,Tanzania Bara na wenyeji Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news