DPP Mwakitalu akabidhi mali za mabilioni zilizotaifishwa kutokana na uhalifu

NA DIRAMAKINI

OFISI ya Taifa ya Mashtaka imekabidhi Wizara ya Fedha na Mipango mali 8,188 zenye thamani ya shilingi bilioni 4.4 bilioni zilizotokana au zilizotumika kutenda uhalifu nchini.
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Sylvester Mwakitalu amekabidhi mali hizo Oktoba 3, 2022 jijini Dodoma kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba ambapo zimekusanywa katika mikoa mbalimbali Dar es Salaam,Mtwara, Njombe, Morogoro, Dodoma na Kagera.

Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Chotto Sendo amesema, makabidhiano hayo yanahusu nyumba 19, viwanja tisa, mashamba mawili, vyombo vya moto 63, magari 31 na pikipiki tisa.SOMA BAADHI YA MALI ZILIZOTAIFISHWA HAPA

Sendo amesema, mali nyingine ni mbao 4,796, madumu 109 ya lita 20 kila moja ya mafuta ya ndege/taa, mashine moja ya kukobolea mpunga na madini ya bati yenye uzito wa kilo 2,104.

Amesema, katika kuhakiki wamekutana na changamoto mbalimbali kwamba kuna mali ambazo zina zaidi ya miaka mitatu,hivyo zimeanza kuharibika lakini vilevile wamiliki wa hizo mali wameendelea kuzitumia.
Naye Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu amesema, awali baadhi ya mali walizokabidhi Serikalini siku za nyuma zilileta changamoto kwa washtakiwa kukataa rufaa na mahakama kutengua maamuzi ya mwanzo.

Mwakitalu amesema hiyo ndio sababu kuu ya mali hizo kuendelea kushikiliwa na ofisi yake kwa kipindi hicho ili kutoa nafasi kwa washtakiwa kutafuta haki zao zote kabla ya kuzikabidhi kwa Serikali.

Pia amesema kuwa, mali wanazokabidhi hazina kipangizi kwa sababu washtakiwa walipata nafasi ya kutafuta haki zao hadi mahakama za juu ama wengine waliridhika na uamuzi wa mahakama.

Amesema, kwa mujibu wa sheria mhalifu hatakiwi kunufaika na mali alizopata kutokana na uhalifu kwa sababu zikibaki kwa wahalifu zitatumika kufadhili uhalifu mwingine au zitawanufaisha wahalifu na kuonesha jamii uhalifu unalipa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema baada ya kukabidhiwa kwa mali hizo watafanya uchambuzi kuona zinazofaa kwa ajili ya matumizi ya Serikali ambazo watazigawa kwa taasisi za umma zikaendelee kutoa huduma na zisizofaa kwa matumizi ya Serikali zitapigwa mnada.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news