GEITA WACHANGAMKIA MRADI WA SAMIA HOUSING SCHEME (SHS)

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Madini,Dkt.Doto Biteko amewataka washiriki wa Maonesho ya Tano ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini kuhakikisha wananchi wanaotembelea mabanda yao wanapata uelewa mzuri wa shughuli wanazozifanya na kuwaeleza kwa kina mipango na mikakati yao waliyojiwekea.
Waziri wa Madini,Dkt.Doto Biteko (mwenye suti nyeusi) na Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella (aliyevaa kofia mstari wa mbele), akipata maelezo katika moja ya mabanda aliyoyatembelea.

Mhe. Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 3,2022 wakati wa ufunguzi wa Maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya EPZA Bombambili mjini Geita,

Amesema kuwa, maonesho haya yatoe elimu ya kina kwa wananchi ili waweze kuwa na manufaa kwao na kujua taasisi ama kampuni inatekelza vipi majukumu yake na kwa makampuni yenye miradi mikubwa na midogo inatumia mbinu gani katika kubuni na kuanzisha na kukamilisha miradi yake kwa wakati.
Mtoto Wisdom Masumbuko mkazi wa Geita (aliyenyanyua kipeperushi juu) akijadiliana jambo na Afisa wa NHC. 

“Niwaombe washiriki wa maonesho haya kuhakikisha elimu tunayotoa kwa wananchi wanaotembelea mabanda yetu inawasaidia kuzifahamu vyema Taasisi zenu ili hata mwananchi huyu anapohitaji bidhaa kutoka kweny basi awe na uelewa mzuri wa kujua bidhaa mnazozalisha zitamsaidia katika hitaji lake alilokusudia,"amesema Dkt.Biteko.

Amebainisha kuwa, pamoja na elimu inayotolewa pia amewataka wananchi kuchangamkia fursa zinazotolewa na washiriki wa maonesho hayo kwa manufaa yao kwani wamerahisishiwa kuzipata huduma hizo kupitia Maonesho ya Madini.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Bw.Martin Shigella, amewakaribisha washiriki wa maonesho hayo kuzitumia vyema fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Geita.

Wakati huo huo wananchi 11 wa mjini Geita na Mikoa ya jirani wamejaza fomu kwa ajili ya kununua nyumba zinazotarajiwa kujengwa katika eneo la Kawe Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam katika mradi ujulikanao kwa jina la SAMIA HOUSNG SCHEME (SHS).
Afisa Mauzo na Masoko Mwandamizi NHC,Bw.Daniel Kure akizungumza na Waandishi wa Habari katika Maonesho hayo.

Ujazaji fomu huo umefanyika na unaendelea kufanyika katika Maonesho ya Tano ya Teknolojia n Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoongozwa na kauli mbiu isemayo “Madini na Fursa za Uchumi: Ajira kwa Maendeleo Endelevu, yanayofanyika katika viwanja vya EPZA Bombambili mjini Geita.

Baadhi ya wananchi waliojaza fomu hizo ni Dakta. Gosbert Rwakatare wa jijini Mwanza amesema, kufuatia taarifa mbalimbali alizozipata kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii amevutika kufika kwenye Maoensho haya ili aweze kupata taarifa rasmi kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo.

“Nimefurahi sana kuliona banda la Shirika la Nyumba la Taifa - NHC nimekuja hapa mahususi kujua napataje nyumba katika mradi wa SAMIA HOUSNG SCHEME, kwanza niwapongeze sana kwa kutuletea mradi huu, kwani michoro na namna mavyoeleza ni wazi kuwa mradi huu utaleta tija sana kwa wote wakaobahatika kujipatia nyumba,” amesema Rwakatare.
Afisa Mauzo na Masoko Mwandamizi NHC Bw. Daniel Kure akiwaonesha wananchi waliofika katika banda la NHC mradi wa viwanja vya Safari City. 

Rwakatare ameongeza kwamba mahali ambapo panajengwa nyumba hizo ni eneo la rafiki hivyo kwa mtu anayehitaji kuwekeza katika sekta ya nyumba hana budi kuchangamkia fursa hii ambayo baadaye itamnufaisha mnunuzi na kuweza kumuongezea kipato kupitia nyumba anayomiliki.

Kwa upande wake, Bw. Joseph Tungaraza ambaye naye amejaza fomu amesema kuwa amevutiwa sana na mradi wa SAMIA HOUSING SCHEME ambao unatoa fursa kwa baadhi ya watanzania ambao walikuwa na ndoto ya kumiliki ghorofa hivyo kupitia mradi huo naye atakuwa miongoni mwa wamiliki wa ghorofa nchini kwa kuwa atamiliki sehemu ya ghorofa hivyo kujiona naye ni mmiliki.

“Kwanza niwapongeze sana NHC kwa kuamua kutuletea mradi huu, mimi ni katia ya watu ambao nilikuwa natamani sana kumiliki ghorofa lakini uwezo wa kujenga sina, lakini kupitia mradi huu nami natarajia mara baada ya kukamilisha malipo na taratibu zote nitakuwa namiliki sehemu ya ghorofa tena katika jiji la Dar es Salaam,"amesema Tungaraza.

Tungaraza alibainisha NHC inatekeleza miradi mingi sana nchini, tunaliomba Shirika letu lisitusahau wakazi wa Geita kwa kutujengea jengo kubwa la biashara kama ambavyo mmejenga sehemu mbalimbali nchini, kwani ukiuangalia Mkoa wa Geita hakuna majengo mengi ya biashara na hata yalipo bei za upangaji ni kubwa kiasi ambapo ninaimani ikiwa NHC mtajenga hapa Geita hata bei za upangaji zitakuwa za kawaida tofauti na za watu binafsi.
Baadhi ya Wananchi waliotembelea banda la NHC wakisaini kitabu cha wageni kabla ya kupata maelezo ya fursa iliyoletwa na NHC katika Maonesho hayo.

Mwananchi mwingine, Bi. Jane Sambwe ameliomba Shirika la Nyumba la Taifa kutoa elimu ya uwekezaji katika sekta ya nyumba kwenye migodi mikubwa na migodo iliyopo mjini Geita kwani wapo wachimbaji ambao wanahitaji nyumba lakini wanashindwa kupata elimu hiyo kutokana na mfumo wa kazi yao, hivyo NHC itumie fursa hiyo kwenda migodini kwa ajili ya kuwaelimisha kwani wapo wanaohitaji nyumba lakini hawana watu wa kuwasimamia vizuri kwenye ujenzi, lakini kama watafahamu uwepo wa nyumba za kuuzwa na NHC basi watachangamkia fursa hiyo kwa haraka.

Shirika la Nyumba la Taifa ni moja kati ya Taasisi inayoshiriki katika Maonesho hayo ambayo pia yamezishirikisha kampuni mbalimbali zikiwemo za madini kwa ajili ya kuonesha na kuwaelezea wananchi shughuli wanazozifanya.

Post a Comment

0 Comments