Tanzania,Czech zakubaliana kuimarisha utalii, biashara na uwekezaji

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya Czech zimekubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano hususan utalii, biashara na uwekezaji ili kukuza na kuimarisha misingi ya diplomasia iliyopo baina ya mataifa hayo.
Kikao baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), amebainisha hayo alipozungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mbarouk amesema Tanzania ilisaini mkataba wa ushirikiano na Jamhuri ya Czech mwaka 2006 hivyo ni wakati muafaka wa kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na ujumbe wa Jamhuri ya Czech unaoongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa.

“Ni muda tangu tuliposaini mkataba wa makubaliano hivyo kwa sasa ni wakati muafaka baina yetu kuingia mkataba wa makubaliano katika maeneo mapya ya ushirikiano hususan katika sekta biashara na uwekezaji, Utalii,” amesema Balozi Mbarouk

Balozi Mbarouk ameongeza kuwa katika sekta ya utalii, miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa inapokea watalii 6,000 kutoka Jamhuri ya Czech, na kwa kuwa maambuzi ya uviko 19 yamepungua duniani, Tanzania imeboresha mazingira ya utalii, biashara na uwekezaji.

Amewasihi watalii na wawekezaji kutoka Czech kuja kutalii na kuwekeza Tanzania.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa amesema Czech inajivunia ushirikiano wake imara na wa muda mrefu na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuwa Czech itaendelea kudumisha ushirikiano huo.

“Nakuahidi kuwa tutaendelea kuwahamasisha watalii, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Czech kuja kutalii na kuwekeza Tanzania…..ni jukumu letu kuhakikisha kuwa sekta ya biashara na uwekezaji inakuwa na kunufaisha mataifa yote mawili,” amesema Mhe. Tlapa

Mhe. Tlapa ameahidi kuwa Czech itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mengine ya ushirikiano kama vile elimu, afya, kilimo, utamaduni na michezo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Tlapa yupo nchini kwa ziara ya kikazi kuanzia tarehe 2 – 4, Oktoba 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news