HGWT yawakutanisha wasichana iliyowapa hifadhi katika mdahalo Serengeti, wafunguka

NA FRESHA KINASA

KUELEKEA Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike Oktoba 11, 2022 Wasichana waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni wanaopatiwa hifadhi katika kituo cha Nyumba Salama Kilichopo Kiabakari wilayani Butiama na Hope Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara wamewahimiza wasichana na wanawake wanaofanyiwa vitendo vya kikatili kujitokeza kupaza sauti zao na kuripoti katika mamlaka za Serikali ili hatua zichukuliwe kwa wahusika, badala ya kukaa kimya na kuviona vitendo hivyo kama sehemu ya maisha yao.
Ambapo kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka 2022 inasema 'Haki zetu ni hatima yetu wakati ni sasa'. Siku hiyo ilipangwa na Umoja wa Mataifa katika kuendeleza harakati za usawa wa kijinsia na kuongeza uwezo wa watoto wa kike pamoja na haki zao kama vile usawa wa kijinsia, haki ya elimu, haki ya kulindwa dhidi ya ubaguzi, haki ya matibabu kuepushwa na ndoa za lazima.
Pia, siku hiyo huelezea mafanikio ya watoto wa kike na wanawake kwa ujumla na kwa mara ya kwanza iliadhimishwa Oktoba 11, 2012.
Wamesema kutowaripoti wanaofanya vitendo vya kikatili ni kuwapa mwanya waendelee kufanya hivyo kitendo ambacho kina madhara makubwa na kinaathiri maendeleo na ustawi bora katika jamii. Na hivyo, wamesisitiza serikali kuendelea kutoa adhabu kali kwa wote wanaobainika sambamba na wadau na jamii kuendelea kukemea vikali suala la ukatili wa kijisia.

Wameyasema hayo leo Oktoba 9, 2022 wakati wa mdahalo uliofanyika katika Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama kilichopo eneo la Misitu wilayani Serengeti ambapo uliandaliwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania na kuwakutanisha wasichana kutoka vituo viwili vinavyomilikiwa na shirika hilo ambavyo hutoa hifadhi kwa wasichana hao.
Solea Marwa kutoka Nyumba Salama Kiabakari Butiama amesema, wapo watoto wa kike ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia na ndugu zao wa karibu katoka katika famia zao, lakini wamekuwa wakiogopa kuripoti katika vyombo vya sheria ikiwemo Polisi, Dawati la Jinsia na Ofisi za serikali za mitaa wakiogopa laana. Hivyo amewaomba kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa hizo bila kuogopa.

Sarah Zabron kutoka Nyumba Salama Butiama amesema, jamii imekuwa ikimchukulia mtoto wa kike kama chombo duni na mtu asiyethaminika sawa na mtoto wa kiume, ameiomba serikali kuendelea kusimamia kikamifu sheria ya mtoto sambamba na kumlinda na kusikiliza malalamiko ya ukatili pindi wanapoyatoa badala ya kukaa kimya na kuona kama sehemu ya maisha yao.
Zawadi Richard amesema, mila ya ukeketaji imeendela kuwa na madhara makubwa kwa wasichana ikiwemo kutokwa damu nyingi, kuwaathiri kisaikolojia na hivyo ameomba ngariba ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya ukeketaji wapewe adhabu kali wanapotiwa hatiani ili kutoa fundisho kwa wengine wanaotamani kuketa watoto wa kike ili kuwaozesha kwa ajili ya kujipatia kipato kinyume cha sheria za nchi.
Amina Ramadhani kutoka Hope Mugumu amesema kuwa, jamii inapaswa kuwapa haki ya elimu watoto wa kike sawa na watoto wa kiume kwani ni msingi wa maendeleo na kuimarisha usawa katika jamii, badala ya kuwaozesha katika umri mdogo na hivyo kukatishwa ndoto zao.
"Naomba pia suala la ushahidi mahakamani lipewe, mkazo kwani wakati mwingine binti anaweza kukeketwa, lakini kesi inapofika mahakamani watu hawajitokezi kutoa ushahidi hili nalo ni tatizo kubwa na pia pawepo mazingira mazuri ya mtoto wa kike aliyefanyiwa ukatili kutoa ushahidi wake na alindwe vizuri,"amesema Amina.
Beatrice Yohana kutoka Nyumba Salama Kiabakari wilayani Butiama amesema, watoto wa kike wanapotimiziwa haki za msingi wanakuwa na hatima njema kwa siku za usoni na kuisaidia jamii kuiletea mabadiliko chanya ya kiuchumi na kijamii ambapo amesema juhudi za kupambana na vitendo hivyo zifanywe na watu wote badala ya kuiachia jukumu hilo Serikali na mashirika.
Fenanzia Mwita kutoka Hope Mugumu ameomba viongozi wa dini kukemea vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kutoa mafundisho ya kiroho na kuonesha namna ambavyo vitendo hivyo ni dhambi kubwa na havipaswi kufanywa kwani vinakiuka maagizo ya Mungu.

Neema Chacha amewashauri viongozi wa vyama vya siasa kuwa sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau wa mapambano ya ukatili wa kijinsia kwa kukemea na kuwafichua wanaofanya vitendo hivyo bila kuwaficha. Na kwamba mila na desturi zilizopitwa na wakati ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni ziachwe na badala yake mila na desturi nzuri ziendelezwe kwa manufaa ya jamii na taifa pia.
Rebeka Joshua ameomba elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia iendelee kutolewa hasa maeneo ya vijiji ambako wananchi wengi hawana ufahamu na uelewa wa haki za binadamu kwa kuwafikia wazee wa kimila na makundi mbalimbali ambayo yakielimishwa yatakuwa na mchango mkubwa wa kufanikisha mapambano hayo.
Mchungaji Steven Kolokoni wa Kanisa la Shekinah Presbyterian Serengeti amelipongeza Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kuendelea kuwasaidia watoto wa kike ikiwemo kuwapa hifadhi wanapokimbia ukatili kutoka katika familia zao na kuwaendeleza kifani na kitaaluma ambapo amesema kitendo hicho kinawawezesha kutimiza ndoto zao.

Huku akisisitiza serikali kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na mashirika na wadau wanaopambana na ukatili wa kijinsia.

Post a Comment

0 Comments