HIZI AJALI ZINGINE-4:Mwendokasi kwetu sio, kwa wengine tujifunze

NA LWAGA MWAMBANDE

UKIWA unaendesha chombo chochote cha moto, hakikisha unaendesha umbali wa kutosha nyuma ya gari lililo mbele yako au chombo kingine ili uweze kuwa katika hali ya usalama na epuka kuendesha mwendo kasi.

Pia yafaa kuepuka hali zinazoweza kukulazimisha kutumia breki ghafla na usiendeshe gari ukiwa na usingizi au chini ya shinikizo. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,usalama wako na watumiaji wengine wa barabarani unategemea utii wako wa sheria bila shuruti, endelea;

1:Maisha yazidi mbio, hivyo bora tuyatunze,
Mwendokasi kwetu sio, kwa wengine tujifunze,
Kutii sheria ndio, huko na tujiongeze,
Hizi ajali zingine, twaweza kuziepuka.

2:Uendako ni kikao, yako twende yasikize,
Pengine yana mafao, mfukoni uongeze,
Barabara yako yao, gari usilikimbize,
Hizi ajali zingine, twaweza kuziepuka.

3:Madereva ni Amani, ni bosi wakusikize,
Mwendo wa madhabahuni, waache watekeleze,
Mbio fupi za nyikani, acha zisiwamalize,
Hizi ajali zingine, twaweza kuziepuka.

4:Viongozi gozigozi, mbio zenu mpunguze,
Kwa madereva ni kazi, ya kwamba muwakimbize,
Jua nyie ni wazazi, majukumu muyawaze,
Hizi ajali zingine, twaweza kuziepuka.

5:Usalama barabara, kazi msiziongeze,
Ajali kwao hasara, kupima wajisogeze,
Na pengine mnakera, njia waingojeleze,
Hizi ajali zingine, twaweza kuziepuka.

6:Sote tukiwajibika, ajali tuzipunguze,
Pazuri twaweza fika, ifike tujipongeze,
Ajali zitapunguka, vifo tusiviongeze,
Hizi ajali zingine, twaweza kuziepuka.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Post a Comment

0 Comments