Malkia Máxima kufanya ziara Tanzania inayoangazia huduma za fedha za kidijitali

NA GODFREY NNKO

MALKIA wa Uholanzi, Máxima atazuru Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia leo Jumatatu ya Oktoba 17, 2022 hadi Jumatano Oktoba 19, 2022 kwa nafasi yake kama Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ujumuishwaji wa mifumo ya fedha kwa maendeleo.

PICHA NA GETTY IMAGES.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa Na.274 iliyotolewa na Kurugenzi ya Huduma za Mawasiliano Serikalini ya Uholanzi.

Ziara hiyo inakuja wakati mwafaka ambapo kwa sasa Tanzania inaandaa Mwongozo wake wa Tatu wa Kitaifa wa Ushirikishwaji wa Kifedha kuhusu upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali kwa Watanzania wote.

Kwa mujibu wa Kanzidata ya Global Findex ya Benki ya Dunia, asilimia 52 ya watu wazima nchini Tanzania sasa wana akaunti ya benki, ikilinganishwa na asilimia 17 mwaka 2011.

Ongezeko hilo linatokana na baadhi ya watu kuwa na akaunti ya benki ya kidijitali. Hata hivyo, inaelezwa bado kuna pengo la asilimia 13 kati ya wanaume wenye akaunti ya benki na wanawake.

Kwa mujibu wa tarifa hiyo, wakati wa ziara yake, Malkia atazungumza na wawakilishi wa Serikali na wa mashirika ya maendeleo ya kimataifa, taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na wadau wengine ili kufahamu ni nini kinapaswa kufanywa ili kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa makundi yaliyoathirika.

Mtazamo utakuwa kwa watu wa kipato cha chini, wanawake na wafanyabiashara wadogo (wakiwemo wakulima). Kwani,katika uchumi wa kidijitali unaojumuisha kila mtu wanafaa kuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu.

Malkia Máxima ataanza ziara yake siku ya Jumanne katika mkoa wa Kilimanjaro. Kwanza atakutana na wakulima wa ndani na wawakilishi wa ACRE Afrika ili kuzungumza kuhusu bidhaa za bima za shirika hilo.

ACRE hutumia takwimu za hali ya hewa iliyotolewa na setilaiti na vituo vya hali ya hewa ili kutathmini hali kwenye shamba na uwezekano wa uharibifu wa mazao.

Wakulima, mara nyingi hususani wadogo bila wafanyakazi, wanaweza kuchagua ni kiasi gani cha bima wanachotaka dhidi ya uharibifu wa mazao kutokana na mafuriko au ukame, kulingana na bajeti na mahitaji yao.

Ziara ya pili itahusu mradi wa MomCare unaotekelezwa na PharmAccess. Hiki ni kifurushi cha huduma ya afya kidijitali chenye gharama zisizobadilika na viwango vya ubora kwa huduma ya afya ya uzazi.

Wanawake wajawazito wanaoshiriki katika mradi huo hupata kadi ya bima ya kidijitali inayowawezesha kuhudumiwa katika hospitali teule wakati wa hatua mbalimbali za ujauzito wao. Takwimu zilizokusanywa wakati wa mradi zinasaidia kuboresha na kurahisisha huduma ya mama na mtoto.

Baada ya ziara hiyo,Malkia Máxima atasafiri hadi jijini Dar es Salaam, ambako atakutana na wachuuzi katika soko la ndani na mawakala wa huduma za benki kwa njia ya simu na kujifunza kuhusu uzoefu wao na huduma za kifedha za kidijitali.

Aidha,Oktoba 19, 2022 Malkia Máxima anatarajiwa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Profesa Florens Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Janet Mbene, Naibu Waziri wa Fedha, na Kundo A.Mathew, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia.

Mada watakazojadili zitajumuisha bidhaa za dijitali kwa umma, kama vile hati za utambulisho, malipo ya kidijitali na faragha ya taarifa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mambo hayo yanachangia matumizi bora ya huduma za kifedha, ujumuishaji na uthabiti wa kifedha,ujumuishi na Mkakati mpya wa Kitaifa wa Ujumuishaji wa Kifedha.

Malkia pia atazungumza na wanachama wa Generation Equality Forum, safari ya miaka mitano iliyozinduliwa mnamo 2021 chini ya uongozi wa UN Women ili kuharakisha maendeleo kuelekea usawa wa kijinsia duniani.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na Mexico na Ufaransa. Nchini Tanzania mkutano huo utahusu njia za kuziba pengo kati ya wanaume na wanawake linapokuja suala la upatikanaji wa huduma za kifedha hapa nchini.

Malkia Máxima pia atazungumza na wawakilishi wa kampuni za teknolojia kuhusu ubunifu wa kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kiuchumi wa kidijitali.

Post a Comment

0 Comments