Rais Samia azindua rasmi matumizi ya majengo mapya Chuo cha Ualimu Kabanga

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 17, 2022 akiwa ziarani Wilayani Kasulu, Mkoani Kigoma amezindua rasmi matumizi ya majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga kilichojengwa na Serikali kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP).
Akizungumza na wananchi wa Kasulu, Rais Samia amesema Serikali imeamua kujenga Chuo hicho ili kitumike kuandaa walimu ambao watakwenda kutumika kufundisha katika shule ambazo zinaendelea kujengwa nchini.

"Leo nimefungua majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga, Chuo kikubwa kilichojengwa kwa ushirikiano na ndugu zetu wa Canada na Chuo ambacho Waziri wa Elimu amekieleza ni Chuo cha Kisasa kinachokwenda kuandaa walimu wengi wa fani zote," amesema Rais Samia.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda Mb) amesema ujenzi wa majengo hayo mapya umekiwezesha Chuo hicho kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi kutoka 400 hadi 800.

Amewataka wana Kigoma hasa wa Wilayani Kasulu kuhakikisha wanatumia fursa ya kuwepo kwa Chuo hicho pamoja na Vyuo vya VETA vya Wilaya kwa ajili ya vijana kupata mafunzo yatakayowawezesha kujenga ujuzi na umahiri.
Naye Mwalimu tarajali wa mwaka wa pili katika chuo hicho, Ester Michael ameishukuru Serikali kwa kujenga miundombonu ya chuo hicho kwani imetatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikitokana na miundombinu chakavu ya majengo ya awali.
Chuo cha Ualimu Kabanga kilijengwa upya baada ya majengo ya awali kuwa yamechakaa na kumilikiwa na kanisa.

Post a Comment

0 Comments