Mapokezi ya Rais Samia mkoani Kigoma yanasadifu ubeti wa utenzi alioimbiwa mara mbili na Dkt.Mohamed Maguo

NA DR.MOHAMED OMARY MAGUO

ZIARA ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Kigoma imedhihirisha na kusadifu ubeti wa utenzi ambao aliimbiwa na Dkt.Mohamed Omary Maguo katika matukio mawili ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambayo Mheshimiwa Rais alikuwa ni mgeni rasmi.
20221018_195018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimia Wananchi wa Mkoa wa Kigoma mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Michezo wa Lake Tanganyika wakati akihitimisha ziara yake mkoani humo Oktoba 18, 2022.

Matukio hayo mawili ni lile la mwaka 2018 la mahafali yaliyofanyika katika Mkoa wa Simiyu na kutanguliwa na kongamano la uchumi wa viwanda na uwekezaji ambapo pia Mheshimiwa Rais Samia alifunguwa kongamano hilo na kesho yake ikawa mahafali.

Tukio la pili ilikuwa ni maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika mwaka 2019 Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo Mheshimiwa Rais Samia alimwakilisha Rais hayati Dkt.John Joseph Pombe Magufuli kama mgeni rasmi katika maadhimisho hayo. Katika matukio haya mawili nilimsomea utenzi nilioandaa na moja ya ubeti ulighaniwa hivi:

_Wengi_ _wanamsifu_
_Kwamba_ _ni_ _mwadilifu_
_Na_ _pia_ _ni_ _nadhifu_
_Pamba_ _anapigilia_

Ubeti huu kitaalamu katika fasihi unasadifu na kusawiri mambo mbalimbali ya maendeleo ambayo Mheshimiwa Rais Samia na serikali anayoiongoza wanatekeleza katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Kupitia ziara yake ya hivi karibuni mkoani Kigoma na pia Kagera na Geita alipata mapokezi makubwa yasiyo ya kifani na wananchi pamoja na wabunge wao wakielezea maendeleo ambayo yamefanyika katika eneo lao ikiwa ni wilaya, tarafa, kata na mkoa kwa jumla. 

Ubeti huu wenye mistari minne umechambuliwa kila mshororo kwa kutumia nadharia ya Simiotiki. Kabla sijaanza kuchambua ni vema nikaeleza kidogo kuhusu _nadharia ya Simiotiki_.

Hii ni nadharia katika uga wa lugha na fasihi ambapo huitazama lugha katika vitu viwili, yaani kitaja na kitajwa au kirejelewa.

Katika mawasiliano kuna kitaja ambalo ndilo jina na kinachotajwa ambacho ndicho kitu chenyewe halisi. Mara nyingi viwili hivyo huwasilishwa kwa kutumia misimbo, picha, ishara na taswira mbalimbali katika kujenga maana na kufanikisha mawasiliano.

Nadharia hii ina misimbo mitano ambayo ni msimbo wa Kiishara, Kiseme, Kimatukio, Kiutamaduni na Kihemenitiki. Misimbo hii mitano ndiyo nyenzo muhimu za kuchambua kazi au matini za kifasihi hasa kipengele cha lugha na namna kinavyowasilisha maana.

Sasa tuone uchambuzi wa kila mshororo kwa kuhusisha na mapokezi ya mheshimiwa Rais Samia katika Mkoa wa Kigoma.

_Mshororo_ _wa_ _kwanza_: " Wengi wanamsifu."

Mshororo huu unapoutazama kijuujuu unaweza kudhani ni sifa za maneno tu la hasha ni sifa za matendo ambayo ameyafanya na anaendelea kufanya katika kuwatumikia Watanzania wakiwemo wana Kigoma. 

Sifa hizo si nyingine bali ni kutokana na shughuli za ujenzi wa miundombinu ya barabara, umeme, maji, afya na elimu ambayo inafanyika nchi nzima.

Kwa Kigoma kwa mfano hivi sasa imeunganishwa na gridi ya Taifa kitu ambacho hakikuwahi kufanyika tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi yetu.

Wilaya mpya kama Kakonko kupata hospitali mpya ya wilaya yenye kila kitu na hivyo kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya karibu na ujenzi wa madarasa mapya ya kisasa ya shule za sekondari na msingi nchi nzima ikiwemo Kigoma ni miongoni mwa mambo ambayo yanathihiri sifa alizopewa mhe. Rais na wana Kigoma kwa mapokezi ya heshima.

Hapa sasa kwa kurejelea msimbo wa kisemi wa nadharia ya Simiotiki tunaona kwamba mapokezi aliyopewa mhe. Rais na kumwagiwa sifa kedekede na watu mbalimbali ni ishara ya kutambua mchango wake katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi wa Tanzania na Kigoma ikiwemo.

Msimbo wa kiseme maana yake ni jambo nasibishi kisemantiki lenye kuonesha kwamba sifa kwa mhe. rais zinazotolewa na watu wengi hazitoki hewani bali zimeegemewa katika kazi za maendeleo zenye kuonekana na zenye kuwanufaisha walio wengi na ndio maana wengi wanamsifu.

Unaweza kujiuliza swali "hawa wengi ni nani?" Bila shaka hawa wengi ni wananchi wa kawaida wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabishara ndogondogo, machinga, bodaboda, mama ntiliye na baba lishe ambao leo hii watoto wao wanasoma bila malipo yoyote kuanzia ngazi ya darasa la awali mpaka kidato cha sita.

" Kwamba ni mwadilifu," huu ni mshororo wa pili ambapo dhana ya uadilifu inafahamika sana na kiongozi bora hupambwa na sifa hii.

Rais Samia anasifika kwa uadilifu na hapa nitatoa mifano michache. Mfano wa kwanza ni ule wa kupeleka maendeleo katika maeneo yote nchini kila mtu anufaike.

Ujenzi wa madarasa 15,000 ulifanyika nchi nzima na sasa mwaka huu madarasa mapya tena 8,000 yanajengwa nchi nzima kila wilaya na kila mkoa. 

Ajira mpya za walimu, madaktari, wahudumu wa afya na watumishi katika kada mbalimbali nchi nzima, kupandisha watumishi madaraja, na nyongeza ya mshahara ni miongoni mwa mambo mengi ambayo mhe. Rais Samia anapata sifa za kumuongezea nguvu ya kujituma zaidi katika kuwatumikia Watanzania.

Kimsingi, Bajeti ya TARURA imeongezwa mara dufu na kila halmashauri imepewa fedha na tumeshuhudia mikataba takribani 900 imeingiwa kati ya TARURA chini ya TAMISEMI na wakandarasi wa ndani kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mijini na vijijini.

Kazi zimeanza na wananchi wa vijijini watapata barabara nzuri zenye kupitika wakati wote iwe jua au mvua. Hakuna sehemu iliyoachwa kila mahali kumepelekewa fedha za miradi ya maendeleo.

Ugawaji wa mbolea na pembejeo kwa wananchi kupitia bajeti kubwa kwenye wizara ya Kilimo ni miongoni mwa huduma kwa wananchi kuwaezesha kujikwamua kiuchumi. Ruzuku kwenye mafuta imendelea kushusha bei ya mafuta na wananchi wanapata nafuu ya maisha.

Sambamba na mifano hiyo hapo juu lakini pia tunaona ujenzi wa vituo vya afya katika tarafa zote ambazo hazikuwa na vituo vya afya. Takribani vituo vipya 200 vimejengwa nchi nzima kwa muda mfupi.

Miradi ya maji nayo inaendelea kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Kigoma kazi inaendelea.

Mikopo ya elimu ya juu imeongezwa maradufu ili wanafunzi wote wenye uhitaji wapate mikopo. Hii ni mifano michache ya uadilifu ambapo Mhe. Rais anafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wananchi wote wanafurahia huduma nzuri na wanapata maendeleo katika maeneo yao walipo. Mapokezi ya heshima Kigoma ni ishara ya kuenzi uadilifu wa mhe. Rais Samia kwa Watanzania. 
Kwa kutumia msimbo wa Kimatukio wa nadharia ya Simiotiki utaona bayana kwamba haya yote yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na mhe. Rais Samia na serikali anayoiongoza ni uadilifu wa hali ya juu ambapo kama kiongozi ameapa kuwa mwadilifu na anatekeleza kwa vitendo.

_Mshororo_ _wa_ _tatu_ unasema, " Na pia ni nadhifu*," ikiwa na maana ya usafi. Hapa kimsimbo kinachorejelewa ni ile hali ya unadhifu kwa maana kwamba ni kuhakikisha wananchi wanapata mambo mazuri, yaani wanaishi kwa raha mustarehe.

Nadhifu ni usafi ni uzuri na kila mtu anapenda kuishi maisha mazuri. Mhe. Rais anapohakikisha huduma za maji zinapatikana, huduma za afya zinapatikana, elimu haiwi kero kwa wazazi kusumbuliwa michango mingi, kuwa na barabara nzuri ni ishara kwamba anawatakia wananchi waishi maisha mazuri yasiyokuwa na bugdha.

Leo mzazi hasumbuliwi ada mpaka kidato cha sita, tayari amepunguziwa msongo wa mawazo na anaishi maisha nadhifu.

Mapokezi ya heshima ya mhe. Rais Samia katika mkoa wa Kigoma ni sadfa ya mshororo huu na hakika katika nchi nzima kazi zinazoendelea kufanyika ni uthibitisho tosha kwamba mhe. Rais Samia anawatakia wananchi maisha nadhifu.

_Mshororo_ _wa_ _nne_ na wa mwisho unasema,

"Pamba anapigilia." Huu ni msimbo wa kiishara ambapo kimsingi haurejelei mavazi bali fikira na maono yaliyopo kwenye akili yake ni kutaka Watanzania wapate maendeleo.

Unaweza ukaliona hili kupitia mifano mbalimbali ambapo Mhe. Rais amefanya jitihada ya kupata mikopo isiyokuwa na riba kabisa hata senti moja ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Tumeshuhudia mhe. Rais Samia akienda katika nchi mbalimbali kuhamasisha wawekezaji na wamekuja wengi na uwekezaji unaendelea. 

Mhe. Rais ameshiriki katika filamu ya, _Royal_ _Tour_ kwa lengo la kuhamasisha watalii na sasa imeripotiwa kwamba watalii wameongezeka maradufu na nchi inaongeza mapato ambayo ndiyo hayo yanayokwenda kwenye miradi ya maendeleo kama ukarabati wa Chuo cha ualimu Kabanga kule Kigoma na vyuo vingine vingi nchi, ukarabati wa shule kongwe na ujenzi wa mpya uanaendelea, mradi wa umeme wa bwawa la mwalimu Nyerere unaendelea, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR umepamba moto, ujenzi wa hospitali za wilaya, rufaa za mikoa na kanda unaendelea na Kigoma imeahidiwa kujengwa hospitali yarufaa ya kanda.

Hivi ni miongoni tu mwa vitu au mambo yenye kuashiria "anapiga pamba" yaani anataka kuona kila sehemu kunasheheni maendeleo na kila Mtanzania ananufaika na matunda ya nchi yake. Ukusanyaji wa mapato na maduhuli kupitia TRA umeimarika sana na sasa zinakusanya Trilioni za kutosha.

Hivyo, kwa muhtasari haya ndiyo yanayosadifu ubeti wa utenzi juu ya Rais Samia kama ukivyotajwa hapo juu na hapa naurejelea tena:

_Wengi_ _wanamsifu_
_Kwamba_ _ni_ _muadilifu_
_Na_ _pia_ _ni_ _mnadhifu_
_Pamba_ _anapigilia_

Ndugu yangu mshititi Dkt.Ahmad Sovu ametoa makala kadhaa kuhusiana na ziara ya mhe. Rais Samia Kigoma, ambazo ni makala nzuri kwa hakika na mimi nikaona niandae sadfa ya mapokezi na yaliyojiri Kigoma kupitia ubeti huo ambao mhe. Rais Samia amewahi kuimbiwa na Dkt.Mohamed Omary Maguo miaka michache iliyopita na leo yanaendelea kudhihiri yaliyofumbatwa katika ubeti husika na siku nyingine panapomajaliwa tutaandaa uchambuzi wa beti nyingine kwa kadri zinavyosadifu masuala mbalimbali yanayofanywa na mhe. Rais Samia na serikali anayoiongoza katika kuwaletea maendeleo Watanzania.

Tunamuunga mkono mhe. Rais endelea kuchapakazi na Watanzania wanashuhudia maendeleo kwani yanawanufaisha wote. Kiu yetu sote ni maendeleo na Mama endelea kutibu kiu hii kwa dozi na dozi za maendeleo mijini na vijijini.

Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mshairi wa Kisasa
Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Post a Comment

0 Comments