NHC yaja na sera shirikishi kwa sekta binafsi, kuzinduliwa Oktoba 21 Dar

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) linatarajia kuzindua Sera yake ya Ubia Oktoba 21,2022 katika Ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JICC).

Uzinduzi huo ni moja ya wapo ya hatua ya mwendelezo wa utekelezaji wa vipaumbele 11 vya shirika ambavyo vinatekelezwa katika mwaka huu wa fedha 2022/23 chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Bw.Nehemiah Kyando Mchechu.

"Kama mnakumbuka mwezi Julai, mwaka huu tulielezea vipaumbele 11 kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 moja ya kipaumbele ni kushirikiana na sekta binafsi kwa maana ya ubia kati yao na NHC.

"Leo nimewaita kuwaelezea kuhusu uzinduzi wa Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa. Sera ya ubia ambayo tunawaalika Watanzania kushiriki ilianzishwa na shirika tangu mwaka 1993 na kufanyiwa maboresho kadhaa kulingana na wakati husika. Maboresho ya mwisho yalifanyika mwaka 2022 na yamezingatia kuvutia uwekezaji kwa kuwa yana maslahi kwa shirika na mwekezaji na yameshapitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika;

Hayo yamesemwa leo Oktoba 11, 2022 na Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Taifa la Nyumba la Taifa (NHC),Bw.Muungano Saguya wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

"Kwa hiyo,shirika sasa linakwenda kuzindua Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa tarehe 21 mwezi huu wa Oktoba 2022, tunakwenda kuwa na tukio hilo muhimu kubwa linakwenda kuishirikisha sekta binafsi na wawekezaji kutoka ndani ya nchi ambao wamealikwa katika uzinduzi huo utakaofanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC) kuanzia saa tatu asubuhi.

"Uzinduzi wa sera hii iliyoboreshwa unalenga kuwa na maslahi mapana kwa shirika, wawekezaji na Taifa kwa ujumla, unalenga kuwapatia fursa wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini,"amebainisha Bw.Saguya.

Amefafanua kuwa, kauli mbiu ya uzinduzi wa sera hiyo ni “Tunajenga Taifa letu kwa Ubia na Sekta Binafsi”. "Kauli mbiu hii inahimiza ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza maeneo yaliyopo katikati ya miji ambayo yana thamani kubwa kuliko majengo yaliyopo sasa ili kukuza mapato ya shirika.

"Katika uzinduzi huu mkubwa tunakusudia kuwa na washiriki takribani 600 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi, vyama na bodi za kitaaluma pamoja na wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi ambao wamealikwa,"amefafanua Bw.Saguya.

Pia amebainisha kuwa,mabalozi wa nchi zenye wawekezaji wakubwa wamealikwa na wawakilishi wa Kamati za Bunge zinazogusa shughuli za shirika wamealikwa pia.

"Kwa mawasiliano zaidi juu ya kushiriki kwenye uzinduzi huo tafadhali piga simu nambari +255 767 566 299 au +255 658 662 800 au tutumie ujumbe kupitia baruapepe nhcjv@nhc.co.tz,"amesisitiza Bw.Saguya.

Amesema, uzinduzi wa Sera ya Ubia unaenda kufungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba. "Na kwa hakika tunaunga mkono maono na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuvutia uwekezaji nchini kwa kuruhusu sekta binafsi ambayo ni injini ya kuleta maendeleo ili iwekeze mitaji yao kujenga uchumi wa Taifa letu,"amesema Bw.Saguya.

"Tangu kuanza kwa utaratibu huu, jumla ya miradi 111 ilitekelezwa ikiwa na thamani ya shilingi Bilioni 300. Katika miradi hiyo, miradi 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 240 imekamilika na kuanza kutumika na miradi 30 yenye thamani ya shilingi Bilioni 60 inaendelea kukamilishwa,"amesema.

Amebainisha kuwa, miradi hiyo imechangia upatikanaji wa ajira, kuboresha mandhari ya miji nchini, kuongeza mapato ya shirika.

Sambamba na kuongeza wigo wa kodi za serikali, kuongeza maeneo kwa ajili ya biashara na makazi na kuipanga miji katika hali ya kuvutia zaidi.

Post a Comment

0 Comments