TAKUKURU yaagizwa kuchunguza matumizi fedha za TASAF

NA JAMES K. MWANAMYOTO

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Ruangwa kufanya uchunguzi wa matumizi ya kiasi cha shilingi milioni 102,080,357.14 zilizotolewa na Serikali kupitia TASAF ili kujenga zahanati katika Kijiji cha Mtakuja wilayani Ruangwa na kuwasilisha taarifa ya uchunguzi huo kwake kabla ya kuhitimisha ziara yake mkoani Lindi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisoma kwa makini taarifa ya ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Mtakuja iliyopo Wilaya ya Ruangwa, inayojengwa kwa fedha za TASAF wilayani humo.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo kwa kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Ruangwa mara baada ya kukagua na kutoridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Mtakuja, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bw. Gaudence Nyamwihura akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea mradi wa ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Mtakuja iliyopo Wilaya ya Ruangwa kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa zahanati hiyo.

Mhe. Ndejembi amesema, amesikiliza kwa makini taarifa ya ujenzi wa zahanati hiyo ya Kijiji cha Mtakuja iliyowasilishwa na mratibu wa TASAF Wilaya ya Ruangwa, lakini hajaridhishwa nayo kutokana na mapungufu yaliyomo ikiwa ni pamoja na kiasi cha shilingi milioni 27 kilichoainishwa kubaki kwenye akaunti kati ya shilingi milioni 102 zilizotolewa na TASAF, hivyo hakitoweza kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Mwonekano wa zahanati ya Kijiji cha Mtakuja iliyopo Wilaya ya Ruangwa ambayo inajengwa kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Kutokana na mapungufu yaliyobainika kwenye taarifa hiyo, Mhe. Ndejembi amemuelekeza Kamanda wa TAKUKURU kuhakikisha anafanya uchunguzi maalum na kumchukulia hatua yeyote akatayebainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akimsikiliza Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Hossea Shibanda, wakati akiwasilisha kwake taarifa ya ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Mtakuja iliyopo Wilaya ya Ruangwa ambayo inajengwa kwa fedha za TASAF.

“Ni lazima tusimamie vizuri fedha za umma hususani za TASAF ambazo zinatafutwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuzikwamua kaya maskini kutoka katika lindi la umaskini, na kuongeza kuwa ni lazima kuwa na uchungu na matumizi mabaya ya fedha za umma,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Hashim Komba akimpongeza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Ruangwa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Hashim Komba ameunga mkono jitihada za Mhe. Ndejembi za kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha zilizotolewa na TASAF kujenga zahanati itakayoboresha huduma za afya katika Kijiji cha Mtakuja, na kuahidi kuwa kamati yake ya ulinzi na usalama itasimamia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa kamanda wa TAKUKURU ili taarifa ya uchunguzi iwasilishwe kwa wakati kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi anaendelea na ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini, pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika Wilaya zilizopo mkoani Lindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news