Tanzania na Qatar watia saini hati za makubaliano

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 6 Oktoba, 2022 ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Chemba ya Biashara ya Tanzania, Zanzibar na Chemba ya Biashara ya Qatar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya Ushirikiano kati ya Chemba ya Biashara ya Tanzania iliowakilishwa na Rais wake, Paul Koyi, Zanzibar iliyowakilishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC), Ali Suleiman Amour pamoja na Chemba ya Biashara ya Qatar iliyowakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Qatar Muhammed bin Ahmed Al Kuwari. Hafla ya utiaji saini wa Mkataba huo umefanyika Doha nchini Qatar.

Kwa upande wa Chemba ya Biashara ya Tanzania, mkataba ulisainiwa na Rais wa Chemba hiyo Paul Koyi, huku pia ukisainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) Ali Suleiman Amour.

Aidha, kwa upande wa Qatar mkataba huo umesainiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya nchi hiyo Muhammed bin Ahmed Al Kuwari uliofanyika jijini Doha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Qatar Muhammed bin Ahmed Al Kuwari pamoja na ujumbe wake, Doha nchini humo tarehe 6 Oktoba, 2022.

Lengo la Mkataba huo ni kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Qatar hususan kwenye sekta za utalii, miundombinu, ujenzi wa mahoteli na usambazaji wa gesi.

Mbali na utiaji saini huo, Rais Samia amefanya mazungumzo na Waziri wa Fedha wa Qatar, Mhe. Ali bin Ahmed Al-Kuwari ambapo wamejadili masuala ya kikodi baina ya nchi hizo mbili, uwekezaji, biashara, gesi, ufugaji, utalii na kilimo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Qatar Muhammed bin Ahmed Al Kuwari mara baada ya mazungumzo, Doha nchini Qatar tarehe 06 Oktoba, 2022. Kushoto ni Rais wa Chemba ya Biashara ya Tanzania (TCCIA) Paul Koyi na kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) Ali Suleiman Amour. (Picha na Ikulu).

Vilevile, katika mazungumzo ya Rais Samia na Waziri wa Afya wa Qatar, Mhe. Dkt. Hanan Mohamed Al Kuwari wamekubaliana wataalamu wa Tanzania wabadilishane uzoefu kwenye sekta ya afya hasa katika huduma za kibingwa na za dharura.

Rais Samia pia katika ziara yake ya kikazi alifanya mazungumzo na Amiri wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al Thani, wafanyabiashara wakubwa na kuhudhuria Mkutano wa Ubunifu wa Afya Duniani (World Innovation Summit for Health) uliomalizika leo katika Kituo cha Elimu cha Multaqa Jijini Doha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news