Programu ya Shule Bora yawaongezea maarifa maafisa habari

NA DIRAMAKINI

PROGRAMU ya Shule Bora imeendesha mafunzo kwa maafisa habari ili kuwajengea uwezo wa kuhabarisha na kuhamasisha umma kimkakati kuhusu maendeleo yanayofanywa na Serikali.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika Kasulu Mji mkoani Kigoma ambapo zaidi ya maafisa habari 26 wa mikoa na halmashauri kutoka mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma wameshiriki.

Akitoa mada wakati wa mafunzo hayo mjini Kasulu, Raymond Kanyambo ambaye ni Meneja Mawasiliano wa Cambridge Education ambayo inasimamia utoaji wa utalaamu kwa programu hiyo amesema,maafisa habari wana uwezo mkubwa wa kuhamasisha na kuhabarisha umma kuhusu malengo na ushiriki wao katika kuboresha elimu ikiwa watatumia vizuri ujuzi waliopatiwa pamoja na uzoefu wao.

"Mafunzo haya ni muhimu kwenu sana, na mkiongeza uzoefu wenu bila shaka Programu ya Shule Bora itafikia malengo yake haraka,"amesema Raymond.

Naye Winfrida Bwire mshiriki wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Habari Wilaya ya Uvinza alisema mafunzo hayo yamemsaidia kupata uelewa mpana wa namna ya kuboresha ufanyaji kazi za mradi huo kwa kuzingatia malengo ya mradi ili kuweza kuboresha elimu ya msingi kwa kutatua changamoto za usambazaji taarifa kwa jamii.

Aidha, Afisa Habari wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Bi.Furaha Kimondo ameushukuru Mradi wa Shule Bora na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kutoa mafunzo kwani yatamuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Shule Bora ni Programu ya Elimu ya Serikali ya Tanzania inayolenga kuboresha elimu ya Awali na Msingi katika mikoa tisa ambayo inafadhiriwa na watu wa Serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la misaada la UK Aid.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo mbalimbali ya kuimarisha uwezo wa wafanyakazi na wadau mbalimbali katika kufanikisha malengo ya programu na Serikali kwa ujumla.

Maafisa habari zaidi ya 110 tayari wamepata mafunzo haya ambao wanatoka katika mikoa tisa inayotekeleza Mradi wa Shule Bora, mikoa hiyo ni pamoja na Dodoma, Singida, Simiyu, Mara, Pwani, Tanga, Katavi, Kigoma na Rukwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news