Waziri Mkenda:Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam itajengwa Kagera

NA MATHIAS CANAL-WEST

KATIKA kuboresha huduma za upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi nchini Serikali imepanga kujenga Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) mkoani Kagera.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema hayo Oktoba 13, 2022 mbele ya mgeni rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya uzinduzi wa Chuo kipya cha Ufundi Stadi na Huduma (VETA) cha Mkoa wa Kagera.
Amesema kuwa, kampasi hiyo itajengwa kwenye vijiji vya Itahwa na Kangabusharo kwenye eneo la ekari 323.45.

Kati ya ekari 323.45 zilizotolewa, ekari 231.36 ziko katika kijiji cha Itahwa na ekari 92.09 katika kijiji cha Kangabusharo.
Akizungumza kuhusu Chuo kipya cha Ufundi Stadi na Huduma (VETA) cha Mkoa wa Kagera, Waziri Mkenda amesema chuo hicho chenye hadhi ya Kimataifa kimejengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa thamani ya Yuani za Kichina Milioni 60.18 sawa na Shilingi za Kitanzania Bilioni 22.4.

Waziri amesema, fedha hizo zinajumuisha shughuli za ujenzi, uwekwaji wa baadhi ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia, mashine na samani katika majengo.

Waziri Mkenda amesema kuwa, chuo hicho chenye karakana, vifaa na miundo mbinu ya kisasa kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya China kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1,400 kwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika fani mbalimbali za ufundi na huduma.

Waziri Mkenda amesema kuwa Chuo hicho cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera kilichozinduliwa na Mhe Rais ni hatua nyingine muhimu katika mpango wa kukamilisha ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya ngazi ya Mikoa.
“Mheshimiwa Rais Tulibakisha mikoa michache sana. Kwa sasa, mikoa mingine ambayo ujenzi unaendelea ni Njombe, Simiyu, Rukwa na Geita na mpango wa ujenzi wa chuo cha Mkoa wa Songwe unaendelea kukamilishwa ili ujenzi uanze,”amesema Prof.Mkenda.

Prof Mkenda amesema kuwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya ngazi ya wilaya ambavyo hadi sasa Wilaya 77 zina vyuo na ujenzi wa vyuo katika Wilaya 62 unatarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha 2022/23 ambapo Serikali imetenga shilingi bilioni 100.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news