Haji Omar Kheri:ACT Wazalendo sikieni,mamlaka ya uteuzi ni ya Rais

NA DIRAMAKINI

CHAMA cha upinzani cha ACT Wazalendo kimetakiwa kutambua kuwa,Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ana mamlaka ya kumteua mtu yeyote ambaye anaona amekidhi vigezo na anafaa kumsaidia kutekeleza majukumu mbalimbali ya kiserikali bila kuingiliwa na maamuzi mengine au kushinikizwa.
Akizungumza mbele ya wanahabari, Bw. Haji Omar Kheri amesema kuwa, mamlaka ya Rais yanampa nafasi ya kuteua watumishi na Bw. Thabit Faina ni mtumishi ambaye kisheria amekidhi vigezo vya kuteuliwa katika nafasi ya utumishi wa juu wa umma.
"Suala la kumfanya kama Rais kakosea kumteua ndugu Faina, si sawa, sababu mamlaka ya uteuzi ni ya Rais, na hata Rais halazimiki kufuata ushauri bali anawajibika kusikiliza ushauri wa ACT-Wazalendo na mtu yoyote anayeshauri."

Bw. Haji Omar Kheri ameenda mbali zaidi na kusema, "Suala la uteuzi wa Bw. Faina na wao ACT-Wazalendo kujitoa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa hayana uhusiano wowote, sababu sheria tumezitunga wenyewe na madai ya ACT-Wazalendo kuwa ndugu Faina aliwaengua wagombea wao si halali, sababu wagombea wao walienguliwa kisheria kwa sababu ya mapungufu ya vigezo na si Faina."amesema.
Bw. Haji Omar Kheri ametumia fursa ya kuonana na wanahabari kuviasa vyama vyote vya upinzani hasa ACT-Wazalendo kutohusisha masuala ya kimamlaka ya Rais kwenye uteuzi na maslahi ya Zanzibar katika serikali ya umoja wa kitaifa, na kudai ya kuwa yeye anaunga mkono teuzi mbalimbali za Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi ikiwemo uteuzi wa Thabit Idarous Faina katika nafasi ya ukurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Post a Comment

0 Comments