Rais Dkt.Mwinyi aita wawekezaji kutoka nchini Kenya,Afrika Kusini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema wakati umefika kwa wawekezaji kutoka nchini Kenya na Afrika Kusini kuja Zanzibar kuwekeza katika sekta za Uchumi wa Buluu, hususani katika Sekta ya Utalii.
Dkt.Mwinyi ametoa wito huo leo Novemba 16,2022 alipozungumza na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Isaac Njenga na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Bi.Noluthando Mayende-Mapele waliofika Ikulu jijini Zanzibar kwa nyakati tofauti kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele katika utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu inayohusisha sekta mbalimbali, kama vile Bandari, Uvuvi, ufugaji samaki, Mafuta na Gesi asilia pamoja na usafiri wa Baharini, huku Utalii ukiwa mhimili mkuu wa kiuchumi.

Amesema, Zanzibar yenye wastani wa hoteli za kitalii 600, ina mahitaji mbalimbali ya bidhaa na vyakula kwa ajili ya hoteli hizo, hivyo akabinisha uwepo wa fursa pana kwa wawekezaji na wafanyabaishara kutoka nchini Kenya kuja nchini kuwekeza katika uanzishaji wa viwanda vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali.

Aidha, Dkt.Mwinyi aliiomba Serikali ya Kenya kutumia fursa ya kuanzisha usafiri rasmi wa vyombo vya baharini kati ya nchi mbili hizo na kusema hatua hiyo itaimarisha mwenenndo wa kibiashara kati ya nchi mbili hizo.

Rais Dkt.Mwinyi amesema ili kufanikisha dhana ya kuimarisha uchumi kupitia sekta ya Uchumi wa Buluu, ni muhimu kuzingatia ushauri wa Serikali ya Kenya unaoazimia kuwajengea uwezo vijana wa Zanzibar, kwa kuwapatia mafunzo katika ngazi mbalimbali kupitia vyuo vya Ubaharia Utalii College vilivyoko nchini humo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsikiliza Mgeni wake Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Mhe.Isaac Njenga wakati wa mazungumzo yao alipofika Ikulu jijini Zanzibar leo kujitambulisha.(Picha na Ikulu).

Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi amesema kuna haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya na Zanzibar katika kukabiliana na changamoto mpya za kiusalama katika Ukanda wa Bahari ya Afrika Mashariki.

Ameeleza ni muhimu kwa vyombo vya usalama kutoka nchi mbili hizo kupanua wigo wa ushirikiano katika kukabiliana na vitendo vya uharamia, usafirishaji wa dawa za kulevya pamoja na ugaidi vinavyojitokeza mara kwa mara katika mwambao wa Bahari ya Afrika Mashariki.

Aidha, amesema kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo kwa kurasimisha matumizi ya Bandari, wakati huu shughuli za kibiashara zikiendelea vyema, hususan kwa wananchi wa Miji ya Mombasa na Vijiji vya Shumba, Mkoa wa Kaskazini Pemba, miji ambayo iko jirani.

Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kushukuru uwepo wa ushirikiano mwema na wa muda mrefu kati ya Kenya na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, huku akiwapongeza wananchi wa Taifa hilo kwa kukamilisha uchaguzi mkuu katika hali ya salama na amani.

Naye Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Isaac Njenga amesema, Kenya imeanzisha miradi mbalimbali ikiwemo uanzishaji wa Chuo cha Mabahari pamoja na Chuo cha Utalii, ili kuwawezesha vijana wa Taifa hilo kupata ujuzi.

Amesema, miundombinu hiyo ni muhimu kwa kutambua kuwa bado kuna rasilimali nyingi za Bahari ambazo hazijafanyiwa kazi kupitia sekta ya Uchumi wa Buluu.

Amewaomba Wazanzibari kutumia fursa ya kujiunga na vyuo hivyo na kupata mafunzo katika ngazi mbali ili kuongeza ujuzi pamoja na kubadilishana uzoefu na wenzao wa Kenya ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya Uchumi wa Buluu.

Aidha, Balozi Nyenga ameomba Serikali ya Zanzibar kuimarisha ushirikiano uliopo katika kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazoukabli mwambao wa Afrika Mashariki, akibainisha nchi hiyo tayari imekuwa na ujuzi wa kutosha kutokana na matukio mbalimbali waliyopitia.

Amesema ushirikiano kati ya nchi mbili hizo ni muhimu kwani pamoja na faida nyinginezo utaisadia kuwadhibiti wahalifu wanaofanya makosa sehemu moja na kukimbilia nchi nyingine.

Amesema ni muhimu kuwepo mafunzo ya pamoja ya kiusalama, hatua aliyobainisha itasaidia kuimarisha na kuhakikisha uwepo wa usalama katika nchi hizo.

Akigusia suala la Uwekezaji, Balozi huyo amesema Wakenya wana hamu kubwa ya kuwekeza hapa nchini na kupongeza uwepo wa hoteli nyingi za kitalii, jambo alilosema linatoa fursa ya kupanuka soko la kibiashara, sambamba na kuibua ajira kwa vijana.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amekutana na kuzungumza na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Bi.Noluthando Mayende-Mapele aliyefika Ikulu jijini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika mazungumzo yao, viongozi hao walijadili mambo mbalimbali ikiwemo haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi uliopo kati ya nchi mbili hizo, kwa maslahi ya wananchi wake.

Pamoja na mambo mengine viongozi hao walipata fursa ya kujadili umuhimu wa kuwahamasisha wawekezaji kutoka Afrika Kusini kuwekeza nchini kupitia sekta za Uchumi wa Buluu, pamoja na namna ya kuongeza idadi ya watalii wanaozuru Zanzibar, sambamba na uwekezaji wenye thamani kubwa katika visiwa vidogovidogo hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news