NA WANYAMA WATUONE, NI UTALII WA NDANI TU

NA LWAGA MWAMBANDE

SEKTA ya Utalii katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatajwa kuwa na mchango muhimu sana katika kuchangia pato la Taifa na kufungua fursa za ajira.

Licha ya sekta hii muhimu si tu kwa wageni kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini,kutuingizia fedha nyingi za kigeni, sisi wenyeji tumekuwa na changamoto kidogo ya kutoupa kipaumbele utalii wa ndani.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, Tanzania imebarikiwa kuwa na hifadhi za taifa, mapori tengefu, fukwe za bahari, utamaduni pamoja na viumbe vya baharini ambavyo pengine hata sehemu nyingine duniani havipo, hivyo tuchange fedha kidogo kidogo nasi tukajionee mambo huko, endelea;


1.Na wanyama watuone,
Siyo sisi tuwaone,
Hebu tukubaliane,
Ni utalii wa ndani.

2.Pesa tuzichangechange,
Na ratiba tuzipange,
Wengiwengi tujiunge,
Ni utalii wa ndani.

3.Siyo kwamba tunapita,
Wanyama waweze pita,
Hata sisi tukipita,
Ni utalii wa ndani.

4.Bora tuhamasishane,
Hata wanne wanne,
Kwa pamoja tukutane,
Ni utalii wa ndani.

5.Nchi itajengwa nasi,
Si kulima mananasi,
Pesa zikuje kwa kasi,
Ni utalii wa ndani.

6.Nchi tuna mbuga nyingi,
Na sehemu nyingi nyingi,
Tutembelee kwa wingi,
Ni utalii wa ndani.

7.Kitaka nenda Mikumi,
Ni wanyama hawaumi,
Wengi tena hawakomi,
Ni utalii wa ndani.

8.Unaijua Ruaha,
Kwa Wahehe siyo Waha,
Tembelea kwa furaha,
Ni utalii wa ndani.

9.Kama wataka wanyama,
Kuwaona siyo noma,
Nao kukuona vema,
Ni utalii wa ndani.

10.Wapendeleaa maua,
Mazuri yanayokua,
Kitulo mbuga chagua,
Ni utalii wa ndani.

11.Katavi kule kwa Pinda,
Tembelea utapenda,
Pundamilia si punda,
Ni utalii wa ndani.

12.Wanyama wakikuona,
Hiyo kwao vema sana,
Na wewe ukiwaona,
Ni utalii wa ndani.

13.Sijaenda kaskazi,
Kule utalii kazi,
Hata kuna wapagazi,
Ni utalii wa ndani.

14.Kama hupendi wanyama,
Tembelea Dasalama,
Huko bandari salama,
Ni utalii wa ndani.

15.Vivutio viko tele,
Tena visivyo kelele,
Tembelea pata shule,
Ni utalii wa ndani.

16.Barabara bora sana,
Dasalamu utaona,
Jiji lawa zuri sana,
Ni utalii wa ndani.

17.Magari yaenda huko,
Hayaji huku ya huko,
Rahisi hata kivuko,
Ni utalii wa ndani.

18.Barabara za angani,
Zisizokanyaga chini,
Dar es Salaam ni nyumbani,
Ni utalii wa ndani.

19.Sasa siyo barabara,
Zilizo juu na bora,
Reli mpya nayo bora,
Ni utalii wa ndani.

20.Kule kusubiriana,
Treni gari hakuna,
Juu chini yapishana,
Ni utalii wa ndani.

21.Kuna viwanja vya ndege,
Kule zinatua ndege,
Tembelea uwakoge,
Ni utalii wa ndani.

22.Hujaiona bahari,
Meli vivuko vizuri,
Tembelea hadi feri,
Ni utalii wa ndani.

23.Soko la samaki feri,
Kuna samaki wazuri,
Pweza wapigwa vizuri,
Ni utalii wa ndani.

24.Majengo yale makuu,
Yale yamepanda juu,
Dar es Salaam iko juu,
Ni utalii wa ndani.

25.Majengo Pacha makuu,
Hiyo ndiyo Benki Kuu,
Yamepaa yako juu,
Ni utalii wa ndani.

26.Bandari Darisalamu,
Maghorofa ni matamu,
Kuangalia ni hamu,
Ni utalii wa ndani.

27.Sasa nisiende mbali,
Daraja lisilo mbali,
Pale Aga Khan ghali,
Ni utalii wa ndani.

28.Daraja kwenye bahari,
Lapendeza siyo siri,
Tembea usisubiri,
Ni utalii wa ndani.

29.Katikati kwenye jiji,
Kama unapata maji,
Na kutafuna soseji,
Ni utalii wa ndani.

30.Ni Ali Hassan Mwinyi,
Barabara siisonyi,
Kunapendeza ninyi,
Ni utalii wa ndani.

31.Majengo kila aina,
Barabara imenona,
Magari yanapishana,
Ni utalii wa ndani.

32.Ufike pale Morocco,
Pazuri ni tetemeko,
Zamani hapakuweko,
Ni utalii wa ndani.

33.Tembea Victoria,
Jinsi panavyovutia,
Jiji letu lavutia,
Ni utalii wa ndani.

34.Kisha uje Makumbusho,
Pale kama uamsho,
Nenda pata mchemsho,
Ni utalii wa ndani.

35.Miji yetu tuione,
Na wanyama watuone,
Uchumi tuchangishane,
Ni utalii wa ndani.

36.Sasa nenda Kaskazi,
Kusini nakupa pozi,
Kilimanjaro ienzi,
Ni utalii wa ndani.

37.Mlima mrefu sana,
Barani kwetu hakuna,
Ule unaofanana,
Ni utalii wa ndani.

38.Kule Ngorongoro chini,
Edeni ya duniani,
Tembeleeni jamani,
Ni utalii wa ndani.

39.Kama ukifika kule,
Uone mandhari ile,
Hutabaki vile vile,
Ni utalii wa ndani.

40.Pale wamuona simba,
Pundamilia atamba,
Wafugaji wanaimba,
Ni utalii wa ndani.

41.Nakwambia kashangae,
Macho yashibe ukae,
Tembea usikatae,
Ni utalii wa ndani.

42.Tanzania yetu tamu,
Kuijua pata hamu,
Tena ufanye kwa zamu,
Ni utalii wa ndani.

43.Usisalie nyumbani,
Waifaidi wageni,
Usiijue wa ndani,
Ni utalii wa ndani.

44.Nenda anzia kusini,
Ufike kaskazini,
Mashariki baharini,
Ni utalii wa ndani.

45.Kule Ziwa Tanganyika,
Magharini kamilika,
Kweli utaburudika,
Ni utalii wa ndani.

46.Kingine sijakisema,
Ni watu walivyo wema,
Ruvuma hadi Kigoma,
Ni utalii wa ndani.

47.Sijataja Visiwani,
Ustarabu nyumbani,
Wala hakuna uhuni,
Ni utalii wa ndani.

48.Niseme mji mkongwe,
Hebu uache utengwe,
Na kutalii ulengwe,
Ni utalii wa ndani.

49.Tuwapendavyo wanyama,
Vile hawawezi sema,
Wanatupenda wanyama,
Ni utalii wa ndani.

50.Twendeni tukatalii,
Tuijui nchi hii,
Iinuke kwa bidi,
Ni utalii wa ndani.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news