SAA 24 ZITUMIKE KUSAFIRI

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 10, 2022 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson ameishauri Serikali kuangalia upya utaratibu uliowekwa katika baadhi ya maeneo nchini wa kuyazuia magari ya abiria kufanya shughuli za usafirishaji nyakati za usiku, jambo ambalo amesema linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi nchini.

Mheshimiwa Dkt.Tulia ameyasema hayo wakati aliposhiriki katika semina kwa wabunge kuhusu usalama barabarani ambayo iliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika Ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Spika amesisitiza ni lazima ufike wakati wananchi waweze kufanya shughuli zao muda wote na kuondoa dhana iliyozoeleka ya magari ya abiria kuwekewa vikwazo.
Amesema, ni shauku ya kila mmoja kuona nchi yetu inachangamka zaidi kiuchumi, hivyo mazuio ya namna hiyo yanakawiza juhudi hizo. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,mawazo ya Spika Dkt.Tulia ni chanya, hivyo saa 24 zitumike kusafiri, endelea;

1:Asante Spika wetu, mawazo yako ni kuntu,
Ya kukuna vichwa vyetu, nchi yetu iwe kwatu,
Ili usafiri wetu, uilete tija kwetu,
Saa ishirini na nne, zitumike kusafiri.

2:Ndiyo hapahapa kwetu, zile taratibu zetu,
Kwa haya malori yetu, kwenye barabara zetu,
Kusafiri hayo kuntu, saa hizo zote zetu,
Saa ishirini na nne, zitumike kusafiri.

3:Na hii misiba yetu, kusafirisha wenzetu,
Kwenye barabara zetu, na haya majonzi yetu,
Muda wote huo wetu, tusijechelewa kwetu,
Saa ishirini na nne, zitumike kusafiri.

4:Na haya magari yetu, binafsi yale yetu,
Twapanga safari zetu, shina nne saba zetu,
Tunapiga moto wetu, bila bughudha na mtu,
Saa ishirini na nne, zitumike kusafiri.

5:Ni vipi mabasi yetu, vizingiti hivyo vyetu?
Mwendo udhibiti wetu, ratiba zao ni zetu,
Mbona tunao ubutu, muda kazi mchache tu?
Saa ishirini na nne, zitumike kusafiri.

6:Ni huyu Spika wetu, ushauri wake kuntu,
Kwamba barabara zetu, zile zisizo na kutu,
Basi na mabasi yetu, yao abiria wetu,
Saa ishirini na nne, zitumike kusafiri.

7:Yale mapungufu yetu, katika sheria zetu,
Au na kanuni zetu, na vyote kikwazo kwetu,
Yaje kwenye Bunge letu, yapitiwe yawe kwatu,
Saa ishirini na nne, zitumike kusafiri.

8:Katika dunia yetu, mashindano ndiyo yetu,
Kama majirani zetu, usafiri si wa kwetu,
Hiyo ni hasara kwetu, uchakarikaji wetu,
Saa ishirini na nne, zitumike kusafiri.

9:Cha muhimu hasa kwetu, hizi taratibu zetu,
Ili usalama wetu, uwe mzuri kwa watu,
Hiyo iwe kazi kwetu, taratibu zile zetu,
Saa ishirini na nne, zitumike kusafiri.

10:Mpira huo si wetu, ni wa mamlaka zetu,
Wao watumishi wetu, haya maslahi yetu,
Wayaamue kiutu, iwe ni faraja kwetu,
Saa ishirini na nne, zitumike kusafiri.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news