Ufaransa yaanza kutetea ubingwa kwa kuichapa Australia mabao 4-1

NA DIRAMAKINI

KATIKA dimba la Al-Janoub, ambao zamani ulijulikana kama Al-Wakrah uliopo Al-Wakrah, Qatar timu ya Taifa ya Ufaransa imewafanya ndivyo sivyo Australia.

Picha na Tolga Bozoglu/EPA-EFE/Shutterstock.

Mabingwa hao watetezi Ufaransa walianza kutetea taji lao la Kombe la Dunia kwa kuicharaza Australia mabao 4-1, huku fowadi mkongwe Olivier Giroud akitengeneza onesho la rekodi katika dimba hilo.

Ni kupitia mtanage wa Kundi D ambao umepigwa Novemba 22, 2022 ambapo Giroud alifunga bao katika vipindi vyote viwili, na kufikia rekodi ya Thierry Henry kama mfungaji bora wa muda wote wa Ufaransa. Bao lake la kwanza alilitupia nyavuni kipindi cha kwanza katika dakika ya 32.

Craig Goodwin aliifungia Australia bao la kuongoza dakika ya tisa, lakini Ufaransa ikahakikisha hakuna fursa tena siku moja baada ya Saudi Arabia kuishangaza Argentina.

Adrien Rabiot alifunga bao la kusawazisha dakika ya 27 kwa mkwaju wa Giroud na kuifanya Ufaransa kuongoza kwa mabao 2-1 hadi mapumziko.

Kikosi hicho cha Didier Deschamps waliongeza mengine mawili katika kipindi cha pili kupitia kwa mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe dakika ya 68 na Giroud akaongeza bao la nne dakika ya 71 na kuwapatia ushindi mnono Ufaransa.

Aidha, kwa matokeo hayo, Ufaransa itamenyana na Denmark katika mechi inayofuata ya Kundi D huku Australia ikikutana na Tunisia. Mechi zote mbili zitachezwa Jumamosi.

Post a Comment

0 Comments