Ukiwa na marafiki wa aina hii, wakimbie kama ukoma 2023

NA DIRAMAKINI

ZIKIWA zimesalia siku chache kabla ya kufunga kitabu cha mwaka 2022 na kufungua kitabu kipya cha mwaka 2023 bila shaka kuna mambo mengi maishani mwaka umeyapitia na unatamani kwa sababu mengine hayakuwa na tija kwako, mwaka mpya ni bora ukayapa kisogo.

Picha na fadhymtanga.

Maisha yetu ya kila siku yanajengwa na marafiki, hii ni kutokana na ukweli kuwa, hawa ni watu ambao tunawaamini kwenye maisha.

Unaambiwa, rafiki ndiye anayeweza kukusaidia au kuacha kukusaidia maana yeye ndiye mwenye kujua siri zako. Hivyo rafiki pia anaweza akawa ndiye adui yako.

Ingawa, mtu ukiwa na rafiki hutakiwi kumshirikisha kila jambo. Lakini, kuna aina nyingi za urafiki, ambazo baadhi yake zinaweza kutofautiana.

Kwani, rafiki anatakiwa awe na upendo, mwenye fadhila, wema, ushujaa, uaminifu, uelewa, huruma, imani na uwezo wa kujitegemea, kuelezea hisia za wengine kwa wengine.

Aidha, tunapoelekea mwaka 2023, moja ya mambo muhimu unayohitaji unapojaribu kuboresha maisha yako ni kuchambua aina ya marafiki wenye nia moja.

Jiulize, marafiki zako wana nia moja kweli? Ili kujua aina za marafiki ambao unapaswa kuwaepuka mwakani, ni pamoja na wenye mambo ya namna hii. Endelea;

Marafiki wenye Wivu

Unashauriwa kuwa, mwaka wako unapoanza haupaswi kuwa na aina hii ya marafiki, kwani katu hawatakutakia mema katika mipango yako, kupitia wivu wao wanaweza kukuharibia mipango yako.

Na mara nyingi marafiki wenye wivu kamwe hawawezi kukubali kukuona ukifanya mambo mazuri ingali wao hawapigi hatua. Aina za marafiki hawa, wanatamani kila jambo ambalo labda ilikuwa riziki yako walipate wao na wewe ulikose.

Pia kwa vyovyote vile ikiwa unaendelea kufanya vizuri maishani, hawatakuwepo kukusaidia. Hawatakuwa na furaha kwako.

Ikiwa unataka kuhisi namna ambavyo hawana furaha kwako, unaweza kuhisi kwa kusiliza mapokeo au sauti zao au nyuso zao zinakupa tabasamu la mashaka, lakini moyoni ni wauaji.

Ukibaini, miongoni mwa marafiki zako iwe kazini au sehemu ya kujipatia riziki wapo wa namna hii, jitahidi unapoanza mwaka mpya kuwapa kisogo, pambana muombe Mungu na bidii yako itakuwezesha kuzifikia ndoto zako.

Zingatia kuwa, watu wenye wivu wana hisia ya kuudhi ndani yao kuelekea mtu mwingine na ni vigumu kwao kudhibiti hisia hiyo.

Marafiki wazushi

Hawa ni aina ya marafiki wanaoeneza uwongo, kueneza uzushi au kutunga uvumi, na kuharibu mafanikio ya wengine.
Marafiki hawa hupenda kusengenya kwa sababu huwapa nafuu ya muda. Wanataka kutafuta sababu ya kujifanya wajisikie bora kwa kusema mambo mabaya kuhusu wengine ili wajisikie wamethibitishwa.

Ni watu wa kiwango cha chini sana ndiyo wanaopenda kwenda na aina za marafiki hawa ambao wana tabia zenye sumu na chonganishi. Ikiwa unataka kuendelea katika maisha na kufikia malengo yako, huwezi kujihusisha na marafiki kama hawa kamwe, jitenge nao na ikiwezekana wakimbie.

Mitazamo Hasi

Marafiki wenye mitazamo hasi, mara nyingi huwa wanahisi kama kila kitu ni kibaya na hakuna kitu kizuri kwake.
Huwa ni wa kwanza kubaini makosa,kwa kila kitu na wao.

Aina za marafiki hawa unaweza kuwafananisha na wingu la giza ambalo likitanda mahali kamwe hauwezi kuona umbali wa upeo wa macho yako, hivyo wingu hilo lilikutanda hautaweza kusonga mbele maishani mwako.

Pia aina za marafiki hawa, huwa wanapenda kuongelea mambo hasi na matatizo halafu baadaye wanashangaa kwa nini wanaendelea kuvutia mambo hasi katika maisha yao.

Ikiwa unataka mafanikio, kitu cha kwanza wape kisogo aina za marafiki hawa wenye mitazamo hasi, nenda na watu wenye mawazo na fikira chanya, lazima utoboe kimaisha.

Mtengeneza matatizo

Marafiki hawa daima hujiweka kwenye matatizo mara kwa mara na watahitaji wewe kuwaokoa. Wanajiingiza kwenye fujo na mambo ambayo yanaweza kuwa ya aibu iwe kazini, jamii au mahali pengine popote. Unaweeza kujikuta unapoteza muda mwingi au rasilimali zako iwe fedha kwa ajili ya kuwapatia suluhu ya matatizo wanayoyatengeneza.

Sio lazima ujihusishe na mtu wa aina hii, kwani watu kama hao wanahasi utu wako. Ikiwa una marafiki wa kutengeneza shida ambao hujifanya wajinga kila wakati, unahitaji kuwaepuka mara moja tena unaweza kuwakwepa kama ukoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news