Yajayo Tamasha la Kimataifa la Bagamoyo yanafurahisha

NA JOHN MAPEPELE

"Naipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ubunifu na mikakati kabambe ya kuandaa matamasha mbalimbali yanayoleta tija kwa wananchi;
Ndivyo alivyosema Rais Samia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Suluhu Hassan, Januari 22, 2022 katikia Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi wakati akizindua Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro lililoratibiwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Chama cha Umoja wa Machifu Tanzania kupitia kwa Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Kilimanjaro, Frank Mareale na serikali mkoani Kilimanjaro.


“Naelekeza mkae pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuja na mkakati wa kuandaa matamasha bora zaidi ili yatumike kuitangaza Tanzania na kutoa ajira kwa wananchi,"aliongeza.
Rais akaweka bayana kuwa, kutokana na umuhimu mkubwa wa utamaduni, aliamua kuunda wizara maalumu ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kutunza maadili, kuzalisha ajira na kukuza michezo na kuwachagua viongozi vijana kuongoza wizara hiyo.

Alisisitiza kuwa, viongozi vijana wanaosimamia wizara hiyo, wanaiongoza kwa ubunifu na ufanisi mkubwa kwani katika kipindi kifupi, wizara imefanya mapinduzi makubwa kwenye sekta hizo na kutaka kuendelea kushirikiana na wadau ili kuboresha zaidi.
Mkuu wa nchi akayataja baadhi ya matamasha ya kihistoria ya utamaduni yaliyoratibiwa na wizara kwa ubunifu wa hali ya juu baada ya Serikali yake kuingia madarakani kuwa ni pamoja na Tamasha la Utamaduni la Bagamoyo, Tanga, Tamasha la Machifu la Utamaduni la Mwanza na Morogoro.

Rais nasisitiza kuwa, serikali yake itaendelea kuimarisha bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuendelea kubaini, kulinda na kuendeleza utamaduni wa Mtanzania kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Wakati akizungumza na viongozi na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Wanawake (Twiga Stars) baada ya kupokea Kombe la Ubingwa wa COSAFA kwa Timu hiyo Oktoba 27, 2021 Ikulu Dar es Salaam, Samia aliwataka watendaji katika wizara na wadau mbalimbali wa sanaa, utamaduni na michezo kushirikiana kufanikisha Tamasha la 40 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo.

Tamasha hilo lilifanyika Oktoba 28- 30, 2021 katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, (TaSUBa).

Kwa kuitikia mwito huo wa Serikali, Wizara imekuwa ikiweka mikakati kabambe kuhakikisha inaboresha matamasha haya kila mwaka ili kuyafanya yawe na tija zaidi kwa taifa.
Katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa alisisitiza kuwa, katika mwaka 2022/23 wizara imejipanga kutekeleza kwa kasi na weledi maelekezo yote 16 ya kisekta yaliyotolewa na viongozi wakuu wa serikali.
Maelekezo hayo ni pamoja na kuandaa na kuboresha Tamasha la Kimataifa la Bagamoyo ili kuwahudumia wananchi.

"Kila mmoja awajibike kwenye eneo lake, tukijifungia ofisini hatutafikia malengo na matarajio ya Serikali… Twende tukawahudumie wananchi, tukawafikie na kuwapa faida ya Serikali yao," alisema Waziri Mchengerwa katika Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika Dodoma Machi 21, 2022.
Miongoni mwa maelekezo makuu yaliyotolewa na viongozi wakuu ni pamoja na kuhakikisha matamasha ya utamaduni yanafanyika kuanzia ngazi ya mtaa, wilaya, mkoa hadi ngazi ya kitaifa na kuimarisha masuala ya hakimiliki kwa wasanii.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa katika kuendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali Wizara kwa kushirikiana na wadau imeandaa Tamasha la 41 la Kimataifa la Bagamoyo litafanyika Novemba 10-12 Bagamoyo likitarajiwa kubwa na la kihistoria.

Kwenye tamasha hili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atawakilishwa na Makamu wa Rais, Dkt.Philip Mpango.

Katika mkutano na Wandishi wa Habari mwishoni mwa juma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi, anasema maandalizi yote muhimu yamekamilika.
Anasema katika tamasha la mwaka huu, kumekuwa na ushikiri mkubwa zaidi wa nchi mbalimbali duniani ikilinganishwa na mwaka jana.

"Tayari vikundi mbalimbali vimeanza kuwasili na vinajinoa kwa ajili ya tamasha hili, tutarajie mambo makubwa,"anasisitiza Dkt.Abbasi.

Mwandishi ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Anapatikana kwa 0784441180 au jmapepele1@gmail.com.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news