Kuwaenzi waasisi wa Taifa letu ni thawabu kubwa, kongole Mheshimiwa Mchengerwa

NA GODFREY NNKO

MWAKA 2021 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipata rais wake wa kwanza mwanamke, Mheshimiwa Dkt.Samia Hassan Suluhu wa Awamu ya Sita.

Rais Dkt.Samia aliingia madarakani baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli mwanzoni mwa mwaka jana.

Ni wazi kuwa, msingi thabiti wa kikatiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulifungua njia kwa matukio kama haya ya kihistoria kutokea nchini na pengine Ukanda wa Afrika Mashariki.

Ikiwa ni zaidi ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) kabla ya muungano wake na Zanzibar mwaka 1964, watu mashuhuri walioshiriki kikamilifu katika mapambano ya Uhuru ni wengi na kwa masikitiko hawaelezwi, zaidi utasikia mmoja tu au wawili.

Changamoto hiyo huwa inajitokeza katika wakati ambao, vizazi vya sasa na vijavyo vinapaswa kuelezwa na kupewa nafasi ya kusherehekewa kila wakati michango ya waasisi wetu ambao wengi wametangulia mbele ya haki.

Miongoni mwao ni Bibi Titi Mohamed, mama huyo alikuwa ni mmoja wa mashujaa ambaye jina lake lilisadifu kile ambacho alikuwa anakitenda wakati huo kwa Taifa, kila mmoja wetu anatambua kuwa,mama huyo alikuwa na upendo kwa Taifa na watu wake.

Bibi Titi Mohamed ambaye alizaliwa mwaka 1926 kwenye familia ya Kiislamu. Kama wenzake wengi wa wakati huo, hakupata elimu kubwa, lakini alijifunza mengi kutoka kwa wazazi wake na familia yake kwa ujumla.

Kila wakati kabla ya hotuba ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Hayati Baba wa Taifa), Bibi Titi alikuwa akiimba ili kuwahamasisha watu wasikilize, ndiyo maana tunaweza kusema kwamba, nyuma ya mafanikio ya Mwalimu Nyerere alikuwa Bibi Titi.

Pia katika miaka ya 1950, alikuwa ni miongoni mwa wale waliopigania uhuru wa Tanganyika kutoka ukoloni wa Uingereza akiwa pamoja na Mwalimu Julius Nyerere chini ya Chama cha Tanganyika African National Union (TANU).

Inaelezwa kuwa, Tanganyika ilipopata uhuru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye aliyesifiwa na kupewa jina la Baba wa Taifa tu.

Lakini bila ya Bibi Titi Mohamed, asingekuwa na ushawishi wa kutosha wa kufanikiwa kuikomboa Tanganyika katika mikono ya wakoloni.

Aidha,Bibi Titi alikuwa ni mwanamke wa kwanza kujiunga na harakati mbalimbali za kupigania uhuru wa Tanganyika. Mwanzoni mwa harakati zake za kisiasa, alifanikiwa kulishawishi kundi kubwa la wanawake kujiunga pamoja naye.

Kama kiongozi wa tawi la wanawake la chama cha TANU, alikuwa na jukumu la kuwashawishi wanawake kuunga mkono maoni na sera za TANU.

Pia baada ya uhuru wa Tanganyika na katika miaka ya mwanzo ya kuundwa kwa Tanzania, muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Bibi Titi alipewa uwaziri chini ya uongozi wa Rais Nyerere.

Harakati za Bibi Titi zilimsababishia hata kuachwa na mume wake, lakini hakurudi nyuma alisimama kidete, hadi anakuwa mwanasiasa mkubwa ndani ya Taifa na mzalendo.

Hadi anavuka mipaka ya nchi na kwenda nje, ndiyo maana unaweza kuona wazi kuwa,Bibi Titi alitoa fundisho kubwa kwa Watanzania ambalo lazima tumuenzi.

Sauti yake na ujasiri wake ulipendwa na wengi, Tom Mboya na Jaramogi Oginga Odinga ambao walikuwa viongozi mashuhuri wa kupigania uhuru nchini Kenya, na miongoni mwa viongozi waanzilishi wa KANU.

Waliomba ushiriki wa Bibi Titi katika mikusanyiko ya kisiasa ya Uhuru nchini Kenya. Alishiriki katika mikutano ya kisiasa mathalani kule Nairobi, Mombasa,Machakos na Kisumu.

Ujumbe wake akiuelekeza kwa wakoloni (Uingereza) kumwachilia huru Mzee Jomo Kenyatta; ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza wa KANU na baadaye akawa rais wa Kenya, lakini alifungwa jela kwa uhaini.

Sauti yake nchini Kenya ilikuwa na athari chanya na ilisababisha wanaume na wanawake kuungana tena katika kupigania uhuru wao.

Jomo Kenyatta alipoachiliwa miaka ya baadaye, alikuja Tanzania kuzungumza mbele ya Watanzania pale Jangwani, Dar es Salaam ambapo alimshukuru Bibi Titi na Watanzania kwa msaada wao.

Kwa kutambua mchango na umuhimu wa Bibi Titi Mohamed kwa Taifa letu, Desemba 14 hadi 15, 2022 Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Rufiji chini ya Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa iliandaa Bibi Titi Memorial Festival katika Uwanja wa Ujamaa Rufiji.

Tamasha hilo ambalo lilijumuisha kongamano la kumuenzi Bibi Titi, burudani na simulizi mbalimbali ambazo zinamuhusu Bibi Titi liliwaleta pamoja mamia ya watu wakiwemo wageni kutoka nje ya Rufiji ambao walipata wasaa wa kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo utamaduni wa wana Rufiji huku wengi wao wakifarijika na upendo wao.

Upendo na ukarimu wa wana Rufiji unasadifu kile ambacho alikuwa nacho bibi yetu Bibi Titi Mohamed ambaye kwa nyakati zote za maisha yake hapa dunia, upendo kwa watu ulikuwa ndiyo msingi wa maisha yake.

Kufanikishwa kwa tamasha hilo kwa mwaka wa pili sasa,kunawafanya wana Rufiji kukiri wazi kuwa, Mbunge wao Mheshimiwa Mchengerwa amekuwa miongoni mwa viongozi wachache ambao wanaamini kutenda kwa kujifunza kutoka kwa waasisi wa Taifa letu ili palipokuwa na ushauri mwema aufanyie kazi kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji mkoani Pwani, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa anafafanua kuwa, utamaduni wa kuendelea kuwaenzi waasisi wa Taifa ni miongoni mwa siri ya kipekee inayosaidia kuharakisha maendeleo katika nyanya mbalimbali.

Pia Mheshimiwa Mchengerwa anasema kuwa, huko awali kulikuwa na tatizo kidogo la kutokumbuka kazi kubwa na kazi nzuri ambazo zilifanywa na waasisi wa Taifa letu.

Anaibainisha kuwa,wapo watu wengi walifanya kazi kubwa na kazi nzuri, ambao kwa bahati mbaya hatukuwa na desturi nzuri ya kuandika historia zao,hata kuwakumbuka na ikumbukwe kuwa hakuna Taifa lolote ambalo linaweza kupiga hatua kama litasahau kazi kubwa na nzuri zilizofanywa na wale waliotutangulia.

Mheshimiwa Mchengerwa anasema, jambo hili linatukumbusha kwamba ili uweze kupiga hatua nzuri hata kimaendeleo lazima ujifunze yale yaliyofanywa na waasisi wa Taifa hili, pale ambapo walitoa elimu na maelekezo ni kuangalia uweze kujirekebisha, kujifunza na uweze kupiga hatua kwenda mbele.

Anasema, tunamkumbuka Bibi Titi Mohamed na ikumbukwe tu kwamba harakati za kumkumbuka Bibi Titi Mohamed zilianza na Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mheshmiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, yeye ndiye aliona umuhimu na mchango mkubwa uliofanywa na Bibi Titi Mohamed na wao wananchi wa Mkoa wa Pwani hawakuwa na ajizi, wakasema kwamba wamkumbuke Bibi Titi Mohamed.

Pia anasema, mwaka jana walifanya sherehe kubwa katika Mkoa wa Pwani katika Wilaya ya Rufiji ambapo ndipo uzazi wa Bibi Titi Mohamed ulipo.

"Ni hapa Rufji. Yeye (Bibi Titi) alikuwa Mbunge wetu wa kwanza katika Mkoa wa Pwani, lakini mbunge wa kwanza katika wilaya hii ya Rufiji.

"Leo tuna mengi ya kujifunza ukiisoma historia ya Bibi Titi Mohamed, ukiadithiwa historia ya Bibi Titi Mohamed utajua alikuwa mtu wa aina gani, alikuwa mtu mzalendo kila Mtanzania analo jambo la kujifunza sio wanawake tu hata sisi vijana wa kiume, alikuwa shupavu, jasiri, mtu aliyetamani kuona kila mtu yuko huru.

"Inawezekana kabisa mafanikio ya nchi yetu leo yanatokana na kazi kubwa iliyofanywa na waasisi wa taifa letu akiwemo Bibi Titi Mohamed ambaye alikuwa mstari wa mbele bega kwa bega na Mwalimu Nyerere,"anafafanua Mheshimiwa Mchengerwa.

Mheshimiwa Mchengerwa anasema, Bibi Titi alikuwa kiongozi wa kwanza mwanamke hapa Tanzania, lakini kule nchini Kenya wakati wa kudai Uhuru kule alikuweko akihamasisha wanawake na alikwenda mpaka Zanzibar akihamasisha akiwataka viongozi kwamba hawawezi kufanikiwa iwapo wanawake watabaki nyuma.

Akasema wanawake watoke majumbani waende wakafanye siasa kwa sababu ya ushawishi walionao, ukweli wao na nguvu walionayo katika jamii.

"Sisi vijana tunajivunia sana, sisi ambao tulipata bahati ya kumuona Bibi Titi Mohamed, sisi ambao tumeweza kusoma na kujionea historia namna ambavyo harakati za ukombozi, namna ambavyo alikuwa mzalendo, mkweli akiamini analoliamini akimhamasisha kila mmoja wetu kudai Uhuru akimtaka kila Mtanzania kipindi kile Tanzania Bara ajiunge na TANU ili kwenda kudai Uhuru.

"Kwa hiyo yapo mambo mengi ya kujitoa mhanga kwa ajili ya taifa lake na mengine mengi kwa ajili ya maendeleo Bibi Titi aliyahamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili wakati ule wa miaka ya 60, kipindi kile Bibi Titi bungeni akiwa anadai wakazi wa eneo fulani waweze kupatiwa taa za barabarani lipo neno alilolisema ambalo Mwalimu Nyerere akiwa Waziri Mkuu alihakikisha anahamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili.

"Lipo neno alilitumia ambalo lilihamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani ya Bunge haya yote na mengine mengi tukisema tuyaeleze tutakesha,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Mchengerwa.

Anasema, haya yote yalifanywa na Bibi Titi Mohamed na wao wanatamani kwamba mchango wa waasisi hao, mchango wa mwanamke ulikuwa mkubwa ukimuacha Bibi Titi Mohamed wapo wanawake wengine wengi katika orodha ambao mchango wao hautambuliwi, wanatambuliwa tu baadhi ya wanaume, ingawa hao wanawake walifanya kazi kubwa sana.

Pia anasema, wako wengi hawatambuliwi, na wengine historia zao hazijaandikwa, hivyo kama Taifa tunayo kazi kubwa sana kila mmoja wao historia zao ziandikwe ziweze kutunzwa vizazi na vizazi miaka 200, miaka 300, miaka 500.

Anasema, tusipoyafanya haya leo vizazi vyetu havitajua kwamba tulipokwenda kupigania uhuru mambo gani yalifanyika, ushawishi gani tuliufanya nani alikiwa mstari wa mbele.

"Wako wengi ambao walifanya makubwa, lakini pasipo kuandikwa historia zao zitapotea kuna umuhimu mkubwa sana kuandika historia yao kuwa na siku yao kuwakumbuka na sisi tumeshaamua tutakuwa na siku maalum kumkumbuka Bibi Titi Mohamed na tumekubaliana na wenzetu ndani ya chama...

"Tunakumbuka uzalendo na ujasiri kutoka kwake kutokana na msingi thabiti yeye na viongozi wengine walituachia, Bibi Titi alikuwa Mbunge wa kwanza hapa kwa hiyo ametufunza mengi ule ujasiri wake wa kujenga hoja, kutenda haki na kuharakisha maendeleo leo tuna barabara ya Kilwa Road, barabara hii ilijengwa kwa kumuenzi Bibi Titi Mohamed.

"Leo ina lami, Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Mwinyi alijenga hii kumuenzi, leo pia Kuna mitaa mingi Dar es salaam na sisi tumekubaliana kwamba pamoja na kuwa na siku maalum tunakwenda kuandika haya yote ambayo tumeyazungumza kwa maneno, lakini hayajaandikwa yako mengi sana,"amebainisha Waziri Mchengerwa.
Jitihada hizo ziliufanya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambao uliasisiwa na Bibi Titi Mohamed, chini ya Mwenyekiti wake wa Taifa kwa sasa, Mary Chatanda kutoa cheti maalum cha pongezi kwa Mbunge na Waziri Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa kwa namna ambavyo anamuenzi Bibi Titi kwa kuwaleta pamoja wananchi na wadau mbalimbali.

Pia alitoka cheti kingine kwaWizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa namna ambavyo inaenzi na kudumisha michango mbalimbali ya waasisi wa Taifa letu, kwa nyakati tofauti.

Katika mahojiano na DIRAMAKINI, baadhi ya wananchi wilayani Rufiji wamekiri kuwa, tamasha hilo limekuwa sehemu ya wao kujitengeneza kipato na kukuza uchumi kupitia mzunguko mkubwa wa fedha.

Aidha, wengi wao wanaonekana kuwa na shauku ya kushuhudia matukio mengi mema ya namna hiyo huku wakishauri kuwa, katika kipindi hiki ambacho Rufiji inaendelea kufunguka kwa kasi kiuchumi ikizingatiwa tayari wameanza kuwa na taa za barabarani, barabara na miundombinu ya kisasa kuna umuhimu wa uwekezaji mkubwa kufanyika.

Uwekezaji huo ambao wanatamani kuuona ni pamoja na nyumba za kulala wageni za kisasa,stendi kubwa, maeneo ya kutolea huduma za kifedha, viwanja na kumbi za kisasa.

Pia kuwepo maeneo mapya na makubwa kwa ajili ya kujipatia vyakula na viburudisho ili kuendelea kuupa hadhi mji wao na ikiwezekana tamasha lijalo mji uweze kumudu kutoa huduma zote zikiwemo za malazi kwa kila mgeni.
 
Aidha, wameshauri Makumbusho kubwa na ya kisasa inayomuhusu Bibi Titi Mohamed ijengwe wilayani humo ili kuendelea kuenzi historia yake na watalii wengi au wageni wakiwemo wenyeji wafike kujifunza.

Kumbuka kuwa, Rufiji ni mahali pa zuri pa kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo ikizingatiwa kuwa, ardhi yake ni kubwa na yenye rutuba ya kutosha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news