Serikali yaripoti visa vipya 442 vya UVIKO-19 nchini

NA DIRAMAKINI

SERIKALI imetangaza mwenendo wa ugonjwa wa UVIKO-19 nchini kwa kipindi cha Oktoba 29 hadi Desemba 2, 2022 huku takwimu zikionesha wanaougua wakiongezeka nchini.

Kuendelea kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara, kuvaa barakoa ni moja wapo ya njia ya kujikinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya UVIKO-19.

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof.Tumaini Nagu kupitia taarifa aliyoitoa Desemba 5, 2022 amefafanua kuwa, visa vipya vya maambukizi ya UVIKO-19 vilivyobainika ni 442.

Amesema, kwamba idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na takwimu za mwezi uliopita ambapo kulikuwa na visa vipya 272, sawa na ongezeko la asilimia 62.5 na kwa kipindi hiki hakuna mgonjwa aliyelazwa wala kifo.

“Serikali imeendelea kutoa huduma za chanjo ya UVIKO-19 nchini ili kuwawezesha wananchi kupata kinga kamili na hivyo kuzuia kupata ugonjwa mkali na hata kifo pale mtu anapopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha UVIKO-19,”amefafanua Mganga Mkuu wa Serikali kupitia taarifa hiyo.

Pia amesema, hadi kufikia Desemba 2, mwaka huu, jumla ya watu 29,123,387 kati ya walengwa 30,740,928 ambao ni sawa na asilimia 94.7 wamepata dozi kamili ya chanjo ya UVIKO-19 nchini.

“Wizara inawahimiza watu wote wenye dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile homa, mafua, kikohozi, mwili kuchoka, maumivu ya viungo, kuumwa kichwa, vidonda vya koo, kupumua kwa shida kwenda vituo vya kutolea huduma za afya mapema ili kuweza kupimwa na kupatiwa matibabu stahiki,"taarifa ya Mganga Mkuu wa Serikali imefafanua.

Mganga Mkuu huyo wa Serikali amefafanua kuwa, Wizara ya Afya inaendelea kutoa tahadhari kwa wananchi wote kuchukua hatua za kujikinga na UVIKO-19 na magonjwa mengine ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na kupata dozi kamili za chanjo ya ugonjwa huo.

Sambamba na kuvaa barakoa pindi unapokuwa na dalili za mafua au kikohozi na uwapo kwenye mikusanyiko mbalimbali.

Aidha, Serikali imesisitiza kuendelea kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara, kuendelea kuchukua hatua za kujenga mwili imara kwa kufanya mazoezi na kula vyakula bora.

Ikiwemo kujenga tabia ya kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya endapo utajihisi wewe ni mgonjwa, au mwingine unaweza kutoa taarifa za kuwepo watu wenye dalili za magonjwa katika jamii kupitia namba ya simu ya bure ya 199 muda wote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news