Wanaume semeni mnapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia-DCP Nzuki

NA MWANDISHI WETU

WANAUME wilayani Mbulu Mkoa wa Manyara wametakiwa kufunguka na kutumia Dawati la Jinsia na Watoto kutoa taarifa pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kupigwa na wake zao.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Naibu Kamishna wa Polisi, DCP Maria Nzuki wakati wa ufunguzi wa Ofisi za Dawati la Jinsia na Watoto zilizojengwa kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu na Afya ya Uzazi (UNFPA) kwa kushirikiana na Shirika la Utu wa Mtoto (CDF).

DCP Nzuki amesema, wanaume wengi wamekuwa wakiona aibu kuripoti matukio hayo katika Dawati jambo ambalo limekuwa likiendeleza vitendo hivyo katika jamii hivyo ili kukomesha tabia hiyo wanapaswa kutoona aibu.

Aidha, alisema mpaka sasa kuna madawati 420 ambayo yanaendelea kutoa huduma nchini na kwa mkoa wa Manyara yapo matatu ambayo yamejengwa katika Wilaya za Simanjiro, Kiteto na Mbulu ambapo kwa kushirikiana na wadau wataendelea kuboresha katika eneo hilo ili kukidhi vigezo vilivyowekwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Sezaria Makota alisema, kufunguliwa kwa dawati hilo ni ishara tosha kuwa vitendo vya ukatili vinakwenda kupungua katika Wilaya hiyo hususani ukatili kwa watoto wadogo.

Makota alisema, baadhi ya Wakazi wa mbulu wamekuwa wakiwaachia babu na bibi katika malezi ya Watoto jambo ambalo linapaswa kukemewa ili wazazi washiriki ipasavyo katika malezi ya Watoto wao.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Manyara Yustina Rahhi alisema, dawati hilo ni mkombozi katika eneo la Mbulu na mkoa wa Manyara kwa kuwa ukatili upo na takwimu siyo nzuri hivyo kila mmoja anapaswa kuchukua hatua katika kukomesha vitendo hivyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news