Waziri Dkt.Mabula awapa tabasamu wagonjwa Sikukuu ya Krismasi

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angeline Mabula amesherehekea Sikukuu ya Krismasi na wagonjwa kwa kula nao chakula pamoja na kukabidhi zawadi mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Waziri Dkt.Mabula amekabidhi zawadi hizo kwa wagonjwa katika wodi ya watoto walio na changamoto ya lishe na watoto walio na changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo watoto waliopata ajali za moto na majanga mbalimbali.

“Nimeamua kuja kusherehekea sikukuu na wagonjwa kwa kuleta chakula nilichopika nyumbani kwangu, vinywaji na matunda kwa sababu najua leo ni siku kuu ya Krisimasi na ushiriki watoto ni muhimu, lakini kuna ambao wameshindwa kusherehekea wakiwa nyumbani kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya,"amesema Dkt.Mabula.

Aidha, Waziri Dkt.Mabula ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ameonesha njia kwa viongozi kusherehekea sikukuu pamoja na wananchi wenye uhitaji ambapo ametoa huduma ya vyakula kwa mikoa yote nchini kwa ajili ya Krismasi na Mwaka Mpya ili watu wote waweze kupika na kusherehekea hata kama hawana uwezo kiuchumi.
“Na mimi ninamshukuru sana Mhe.Rais kwa sababu ameonesha njia toka jana (juzi) mikoa yote amegawa vyakula kwenye vituo vya kulelea watoto kwa ajili ya sikukuu hizi za Krisimasi na Mwaka Mpya, na sisi kama wawakilishi wake ni wajibu wetu kuwatembelea wahitaji hasa watoto ndio maana nimeamua kuja hapa Hospitali kula nao sikukuu,”ameongeza Dkt.Mabula.

Katika ziara hiyo Waziri Mabula aliongozana na Dkt. Ibenzi Ernest Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma ambaye alimshukuru Waziri Mabula kwa sadaka yake hiyo ambayo amesema ni moja katika mchango mkubwa wa mgonjwa kufarijika pale ambapo anaona watu wanamjali.

Dkt. Ibenzi ametumia fursa hiyo kumuomba Waziri Mabula kufikisha shukrani zake kwa Mhe. Rais kwa mafanikio makubwa ya kuboresha huduma za afya hasa katika upatikanaji wa vifaa tiba na maboresho ya majengo ya utoaji huduma za afya katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Kwa kweli sisi watoa huduma za afya tunaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa maboresho mengi yaliyofanyika kuanzia ukarabati majengo, upatikanaji wa vifaa tiba vya kutosha na hata usafi katika wodi zetu, kwani zamani ilikuwa hospitali zina toa harufu kwa kutofanyiwa usafi kwa muda mrefu kwa sababu ya kukosa huduma za vifaa na dawa za kutosha,” aliongeza Dkt. Ibenzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news