Waziri Dkt.Mabula atoa siku 14 kwa kampuni za upimaji ardhi

NA ATHONY ISHENGOMA

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula ametoa siku 14 kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam kukaa na kampuni za upimaji ardhi mkoani humo ili kujiweka sawa kuhakikisha zoezi la urasimishaji jijini Dar es Salaam linakwamuliwa, kwani muda uliopangwa kwa kazi hiyo unakaribia kufikia tamati.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula akisoma maelezo ya hati kabla ya kuanza zoezi la utoaji hati katika viwanja vya Shule ya Msingi Mabagala Kuu jijini Dar es Salaam.

Waziri Dkt.Mabula amesema hayo katika Viwanja vya Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam na kuonya kuwa kampuni za urasimishaji na upimaji wa viwanja ambazo zimechukua fedha za wananchi na kushindwa kukamilisha zoezi hilo zitatakiwa kurudisha madeni, lakini pia kufutwa ili iwe funzo kwa kapuni nyingine ambazo zinafanya kazi kinyume na taratibu na kushindwa kufikia malengo.

Aidha, Waziri Mabula amemtaka Mkurugenzi Manispaa ya Temeke pamoja na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Dar es Salaam kuhakikisha maombi yote ya hati ambayo wananchi wamewasilisha pamoja na kukamilisha malipo yawe yamefanyiwa kazi na wananchi wamepatiwa hati zao ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula ameziagiza halmashauri zote nchini ambazo ni mamlaka za upangaji ardhi kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili ya kupima, kupanga na kumilikisha ardhi badala ya kuachia suala hilo kubaki ni mzigo kwa wizara wakati ni majukumu ya halmashauri kufanya kazi hiyo.

Waziri Mabula pia amepiga marufuku kwa Mkoa wa Dar es Salaam kuendelea kutoa hati zinazozalishwa kwa njia ya analogia kwa wakazi wa Jiji hilo na badala yake watoe hati za kidijiti, kwani mfumo wa ILMIS unafanya kazi, lakini pia akawataka kuendelea kuhuisha kanzi data za ardhi katika mfumo wa kidijitali na kuzitaka halmashauri nyingine nchini kuendelea na zoezi hilo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akimkabidhi hati Mkazi wa Mbagala Kuu Manispaa ya Temeke, Bi. Rashida Azizi Mgaya, hati tano alizokabidhiwa baada ya kukamilisha urasimishaji wa viwanja vyake katika viwanja vya Shule ya Msingi Mabagala Kuu.  

Aidha, Dkt.Mabula ameonya wale wote wanaoendelea na uvamizi katika maeneo ya watu bila kwenda Ofisi za Halmashauri nchini kujiridhisha kuwa wanatenda kosa la jinai na kuonya watendaji kata na vijiji kuacha kuuza ardhi kwani hilo sio jukumu lao bali wenye mamlaka hiyo ni Ofisi za Halmashauri.

Dkt. Mabula ameongeza kuwa wananchi lazima wafuate sheria za ardhi zilizopo na kuonya kuwa kuna baadhi ya watu waliofanya uvamizi na wakatakiwa kulipa mwenye eneo lake lakini wameshindwa kufanya hivyo kwa mantiki hiyo sheria zitafuatwa na kuhakikisha wanatolewa katika maeneo hayo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula pamoja na viongozi wa Manispaa ya Temeke wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi waliofika viwanja vya Shule ya Msingi Mabagala Kuu Kuchukua hati zao mara baada ya kukamilisha taratibu za urasimishaji viwanja vyao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ndata Ludigija aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Temeke katika hotuba yake ya kumkaribisha mgeni rasmi ili aweze kushiriki zoezi la utoaji hati kwa wananchi hao amesema, kuna watu wanapoteza umiliki kutokana na kutopima ardhi suala linalopelekea migogoro ya ardhi kwani kuna baadhi ya wananchi hapa nchini wakijua eneo halina hati wanatengeneza nyaraka feki na kupora mali za wananchi.

Wakati huo huo Kamishna Msaidizi wa Jiji la Dar es Salaam, Bw. Shukrani Kyando amesema zoezi la urasimishaji jijini Dar es Salaam bado linakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa wananchi kuhusu suala la urasimishaji, lakini pia baadhi ya kampuni zinategemea michango ya wananchi hivyo kushindwa kuendesha zoezi la urasimishaji kama ilivyopangwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news