YALIYOSISIMUA 2022: Geordavie, Kuhani na Mwalimu Musa watoa zawadi za magari mapya kwa waimbaji Goodluck Gozbert na Rose Muhando

NA DIRAMAKINI

MOYO wa upendo, ukarimu kwa rika, kabila na itikadi zote,mshikamano na umoja ndiyo vinamfanya Nabii Mkuu Tanzania, Dkt.Geordavie na Kuhani na Mwalimu Musa Richard Mwacha kuwa kati ya viongozi bora zaidi ndani na nje ya Tanzania.

Hivi karibuni, Dkt.Geordavie ameendelea kugusa maisha ya wengi akiwemo Goodluck Gozbert ambaye amemzawadia gari jipya aina ya Mercedes Benz.
Katika hatua nyingine, Kuhani na Mwalimu Musa Richard Mwacha wa Ngome ya Yesu Kristo (Fresh Spring Fellowship) ya Kimara Temboni jijini Dar es Salaam amempatia zawadi ya gari jipya mwimbaji mkongwe na maarufu wa nyimbo za injili nchini, Rose Muhando.

Ngome ya Yesu Kristo ambayo huwakutanisha maelfu ya watu wa dini zote katika ibada za katikati ya wiki na Jumapili imezidi kuwa maarufu zaidi jijini Dar es Salaam kutokana na namna ambavyo watu wamekuwa wakipokea uponyaji wa papo kwa papo.

Gozbert ambaye ni mzaliwa wa jijini Mwanza ambapo kwa sasa anaishi jijini Dar es Salaam ni mwimbaji wa nyimbo za injili kutoka Tanzania. Goodluck anajulikana kwa sauti yake nyororo.
Tangu utotoni mwake, Goodluck Gozbert alikuwa na hamu ya kuimba na kufanya mziki. Katika mahojiano ya hapo awali, Gozbert alisema kuwa hakuwa na nia ya kufuata muziki kama taaluma, lakini kwa sababu ya ugumu wa maisha alilazimika kukuza talanta yake.

Miongoni mwa nyimbo maarufu za Goodluck Gozbert ni Simu, Hasara Roho,
Umeshinda Yesu,Kama si yeye,Ipo siku,
Shukrani Nibaliishe,Mama,Mwenye Majibu,
Pendo Langu,Shukurani na nyingine nyingi.

Katika kipindi chake katika muziki,Gozbert aliteuliwa na kushinda tuzo kadhaa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwaka 2019, alipokea mataji tano wakati wa Tuzo za Maranatha Afrika Mashariki ambazo zinaheshimu matendo bora ya injili kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Ethiopia, Eritrea, na Somalia.

Mnamo mwaka wa 2015, Goodluck Gozbert alishinda Msanii wa Kiume wa Mwaka wa Afrika Mashariki kwenye Tuzo za Sauti, na Msanii Bora wa Injili / Wimbo wa Mwaka kwenye Tuzo za Xtreem. Katika mwaka huo huo, alishinda pia Msanii Bora wa Nyimbo za Injili Tanzania / Wimbo wa Mwaka kwenye Tuzo la Xtreem.

Mbele ya umati mkubwa wa watu chini ya Nabii Mkuu Tanzania, Dkt.Geordavie katika huduma yake ya GeorDavie Ministries Int'l (GDMi) iliyopo Kisongo jijini Arusha, mwimbaji huyo alikabidhiwa gari hilo na fedha taslimu Shilingi Milioni 2 kwa ajili ya mafuta na magurudumu.

Hafla hiyo ilikuwa ni mwendelezo wa dhifa za Kifalme zinazofanyika katika mji wa Daudi chini ya Dkt.Geordavie. Dkt.GeorDavie ni mtumishi wa Mungu, ambaye ameendelea kutumika katika huduma kwa miaka 40 iliyopita.

Ni Rais mwanzilishi na Askofu Mkuu wa kanisa hilo kubwa la Kinabii linalokuwa kwa kasi jijini Arusha, Tanzania na lenye waumini kote Afrika, Ulaya, Marekani na mabara mengine.

Mungu alianza kumtumia GeorDavie tangu akiwa mtoto mdogo. Wazazi wake walimshuhudia akitabiri akiwa na umri wa miaka mitano kwa usahihi sana na mambo yalitokea kadri ya utabiri wake.

Mwishoni mwa miaka ya 70, Mungu alimwita rasmi katika utumishi wa Ufalme kupitia huduma mbalimbali, kuanzia kuongoza sifa na kuabudu, hadi kuwa Mmisionari wa Kitume, Mwalimu wa Biblia, Mwinjilisti, Mchungaji, pamoja na kuanzisha Global Concert Ministries ambapo aliwaongoza vijana katika kukuza vipaji vyao.

Baadaye alianzisha Kituo cha Lighthouse kwa watoto wa mitaani ambapo aliweza kushughulikia changamoto zao na kutoa mwanga katika jamii kwa watoto wa mitaani katika Ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania kwa kuwapatia chakula, nguo, malazi na elimu.

Rose Muhando

Rose Muhando ambaye alizaliwa mwaka 1976 katika Kijiji cha Dumila Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro licha ya kipawa alichonacho kwa ajili ya kumtumikia Mungu, amekuwa akipitia mapito mengi magumu ambayo mengine ni ya kukatisha tamaa na mengine ni ya kumpa nguvu ya kusonga mbele.
Awali, mama huyo alikuwa Mwisilamu na alikuwa ni mwimbaji mzuri sana wa kaswida na alihudhuria kila siku madrasa huko Dumila mkoani Morogoro.

Rose Muhando baadaye afya yake ilianza kudhoofu kutokana na ugonjwa ambao aliangaika kuupima ni ugonjwa gani, lakini hakukutwa na tatizo,hali hiyo ilipelekea maisha kuwa magumu sana.

Ndipo alipoamua kwenda kanisani kwenye maombi, baada ya maombi hayo, alipona na hapo ndipo alipoamua rasmi kubadili dini akiwa na umri wa miaka 12.

Kilichotokea,baada ya kubadili dini wazazi wake kuchukizwa na uamuzi wake,hivyo wakaona ni busara kumfukuza nyumbani kabisa.

Hali iliyozidi kuhatarisha maisha yake na kuendelea kutangatanga na kumsababisha aangukie mikononi mwa wanaume ambao alizaa nao watoto.

Akiwa na mtoto wa miezi sita jijini Arusha aliwahi kufukuzwa na mchungaji kisa alimuomba fedha ili aweze kuingia studio kurekodi kwa kipindi hicho mtoto alikuwa anaumwa ugonjwa wa pumu na alienda Arusha ili aweze kurekodi wimbo wake wa kwanza.

Alianza muziki rasmi katika kwaya iliyopo Dodoma, baadaye akawa mwalimu wa kwaya hiyo ya Dodoma St. Mary’s katika Kanisa la Kianglikana la Chimuli, aliendelea hivyo mpaka alipoamua kuanza kutunga nyimbo zake mwenyewe kwa msaada wa mfuko wa kwaya yao.

Mwana mama huyo ametwaa tuzo mbalimbali ambapo Januari mwaka 2005,alipokea tuzo mbalimbali ikiwamo ya Mtunzi Bora wa nyimbo za Injili, Mwimbaji Bora na Albamu Bora ya Mwaka, zilizotolewa na Tanzania Gospel Music Awards 2004,kupitia albamu yake ya Mteule uwe Macho.

Miongoni mwa albamu zake ni pamoja na Kitimutimu, Uwe Macho,Jipange Sawasawa,Utamu wa Yesu, Yesu Kun’guta na nyinginezo ambazo zimemfanya kuwa shujaa wa injili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news